IRINGA-Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Iramba wilayani Mufindi ambayo inatarajiwa kugharimu sh. bilioni 1.78 hadi kukamilika kwake.
Gharama za ujenzi wa shule hiyo zinahusisha jengo la utawala moja, madarasa nane, ofisi nne, maabara tatu, chumba cha TEHAMA kimoja, nyumba za walimu tani za 2-in-1, bwalo la chakula moja na mabweni manne.
Akizungumza baada ya kufanya ukaguzi wa shule hiyo iliyopo katika kijiji cha Iramba, kata ya Itandula, wilayani Mufindi, mkoani Iringa, leo Jumapili, Julai 07, 2024, Waziri Mkuu amewapongeza madiwani kwa wazo lao la kutenga fedha na kujenga mradi huo.
Waziri Mkuu ambaye yuko mkoani Iringa kwa ziara ya kikazi ya siku nne, ameitaka halmashauri hiyo iendelee kubaini vyanzo vitakavyoongeza fedha ili waweze kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo.
“Moja kati ya mapungufu ya baadhi ya Halmashauri ni kutotumia fedha za ndani kujenga miradi inayoonekana, ujenzi wa shule hii ni mfano wa kuigwa na Halmashauri zote, ongezeni kasi ya mkamilishe mradi huu kwa wakati.”
Pia amewataka watumie vizuri fedha iliyotengwa kwa ajili ya ujenzi wa shule hiyo ili miundombinu yote itakayojengwa iendane na fedha iliyotolewa.
“Fanyeni mapitio ya fedha mliyopanga kutumia kwa ajili ya kujenga nyumba za walimu, shilingi milioni 100 ni nyingi kwa nyumba moja.”
Pia ameagiza madawati yote ambayo hayana eneo la kuweka daftari kwa ajili ya wanafunzi yaondolewe na kurudishwa kwa fundi kwa sababu hayakidhi viwango vya madawati ya shule za msingi na sekondari.
Akitoa taarifa ya ujenzi mbele ya Waziri Mkuu, Mkuu wa Divisheni ya Sekondari wa Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi, Daniele Mapillya, alisema hadi sasa shilingi milioni 363.8 kimepokelewa zikijumuisha shilingi milioni 2.2 ambazo ni nguvu za wananchi na shilingi milioni 361.6 za kutoka kwenye Halmashauri hiyo.
Alisema wameanza utaratibu wa kuisajili shule hiyo ili iweze kutumika kama ya kutwa na isaidie kupunguza umbali kwa wanafunzi wanaosoma kwenye shule mama ya Itandula ambayo ina wanafunzi 1,015.
Wakati huo huo, Waziri Mkuu amekagua ujenzi wa miundombinu kwenye hospitali ya Mji wa Mafinga ambao unahusisha wodi ya wagonjwa wa daraja la kwanza, jengo la kuhifadhia maiti, wodi ya wazazi, jengo la wagonjwa mahututi (ICU) na jengo la kufulia ambavyo vyote vitagharimu sh. bilioni 1.24.