Waziri Mkuu alipongeza Kanisa la TAG kwa kukuza watoto kiimani

DAR-Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amelipongeza Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG) kwa mkakati wake wa kukuza watoto kiimani huku wakilijua na kulishika neno la Mungu.
“Pamoja na shughuli ya uinjilishaji, leo nimeshuhudia watoto wadogo wakisema maneno ya Mungu bila kusoma mahali popote na mwingine akiielezea Misingi ya Kanisa la TAG bila kusoma popote. Hii ni kazi kubwa, mnasathili pongezi.”
Ameyasema hayo leo Jumapili, Julai 14, 2024 wakati akizungumza na viongozi na waumini wa Kanisa la TAG ambako alimwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Maadhimisho ya Miaka 85 yaliyofanyika kwenye uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.

Amesema kanisa hilo linawafanya watu kuwa wamoja, kuwa na uhusiano wa kiimani na kijamii na kutoa mafundisho ya umuhimu wa kushiriki katika huduma kutoa misaada, elimu, huduma za afya na maendeleo ya jamii.

“Kanisa hili ni mfano katika kukuza umoja na ushirikiano kati ya Wakristo wa madhehebu mbalimbali na waamini wa dini nyingine nchini, kitendo ambacho kinatuwezesha kama jamii kuwa na mshikamano na kuimarisha amani na usalama.
Waziri Mkuu amesema Serikali ina kila sababu ya kuwashukuru Wachungaji na Maaskofu kwa kazi yao kubwa ambayo inaimarisha amani, utulivu na maendeleo katika nchi.

“Serikali inathamini mchango wa taasisi za dini katika kuimarisha maadili mema, kukemea maovu na mmomonyoko wa maadili. Wakati wote Serikali imekuwa ikifanya kazi kwa pamoja na taasisi za dini hususani katika kampeni za kijamii za kuelimisha na kuhamasisha maadili mema na mwenendo mwema kwa wanajamii.”

Kwa upande wake, Askofu Mkuu wa Kanisa la TAG Tanzania, Dkt. Barnabas Mtokambali amewataka waumini wa TAG hilo wawe na maono makubwa ya kuweza kulivusha kanisa hilo kwa miaka mingine 85 huku akiweka msisitizo kwa vijana kuyabeba maono hayo.
“Wana TAG ninawasihi tuwe na maono makubwa, tufikiri na kufanya mambo makubwa kwa miaka mingine 85 ijayo. Tuwe na umoja, upendo na mshikamano na tuendelee kujituma na kujidhabihu kwa hali na mali ili mambo makubwa yaweze kutokea,” amesisitiza.

Ametumia fursa hiyo kumpongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na Serikali ya awamu ya sita kwa kazi kubwa anayoifanya Bara na visiwani ya kuiletea nchi maendeleo na hasa kuboresha miundombinu.

Amesema kuanzishwa kwa safari za treni ya mwendokasi kutoka Dar es Saalam hadi Morogoro ni hatua kubwa kwa Serikali katika kurahisisha huduma za usafiri pamoja kuchochea ukuaji wa uchumi.

“Binafsi, ninapoongelea maendeleo, naguswa na hii sekta ya usafiri kwa sababu kwa miaka zaidi ya 10, nimekuwa nikisafiri kati ya saa nne hadi tano kuja Dar es Salaam yalipokuwa Makao Makuu ya TAG.
"Na sasa sasa hivi ofisi zimehamia Dodoma, nimekuwa nikienda huko. Itakapoanza safari za mwendokasi mwezi huu kwenda Dodoma, nitakuwa nimeokoa muda wa saa sita, tatu kwenda Dar es Salaam na tatu kwenda Dodoma,” alisema.

Aidha,ameipongeza Serikali kwa kudumisha amani, umoja, utulivu na uhuru wa kuabudu nchini. “Kutokana na kudumisha haya, imekuwa ni tunu ya kipekee ambayo imeliwezesha kanisa la TAG na madhehebu mengine nchini kupiga hatua kubwa sana za maendeleo.”

Mapema, Katibu Mkuu wa Kanisa hilo, Mchg. Joseph Marwa alisema mbali na majukumu ya kutangaza injili, Kanisa hilo linatoa huduma za kijamii pamoja na kukukuza maadili mema miongoni mwa waumini wake.

“Idadi ya wachungaji imeongezeka, makanisa yameongezeka na kufikia 5,918; wainjilisti wamefikia 2,008; majimbo kwa sasa yako 71 na wilaya ziko 860 kutoka 557 za awali, sawa na wilaya mpya 303.”
Alisema TAG inatoa huduma za jamii kwa kujenga shule za msingi, sekondari, ina vyuo viwili vya ualimu, vituo vya watoto yatima 21, vituo vya kulea watoto 89 na vyuo vya ufundi vitano ambapo kwa sasa chuo kipya kinajengwa Manyara. “Kwa nchi nzima, tumeshachimba visima 293 ikilinganishwa na 153 vilivyo kuwepo zamani,” amesema.

Maadhimisho hayo yalihudhuriwa na Rais Mstaafu wa Benin, Thomas Boni Yayi, Wabunge, wamishenari, viongozi wa makanisa kutoka nchi 13 za Afrika na Asia, viongozi 60 kutoka makanisa ya Kipentekoste, wazee wa imani 10, waangalizi, wachungaji kutoka mikoa mbalimbali na washirika wa TAG.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news