DODOMA-Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ametoa wito kwa taasisi zote za dini nchini kuendelea kushirikiana na Serikali katika kutoa mchango kwenye maendeleo ya taifa.


“Tuna kila sababu ya kuyashukuru Makanisa kwa kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Serikali katika kuleta maendeleo ya wananchi kwa ujumla, yamekuwa sehemu ya suluhisho katika changamoto za kijamii kama vile umaskini, elimu duni, na matatizo ya kiafya.
“Nitumie fursa hii kusisitiza taasisi za dini kuendelea kuimarisha ushirikiano na Serikali na kuendelea kuiishi kwa vitendo kaulimbiu yenu ya Palipo na Umoja, Bwana huamuru baraka! Bwana huamuru baraka, palipo na Umoja.”
Katika hatua nyingine Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa Serikali inathamini uwepo na mchango wa taasisi za dini katika kuhubiri amani na utulivu nchini “Siri ni ya haya yote ni sababu ya uwepo wa dini katika kuhubiri maadili, mshikamano, upendo uvumilivu na kuwa wamoja, Serikali pekee tusingeweza”
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Maaskofu wa Makanisa ya Pentekoste Tanzania (CPCT) Dkt. Barnabas Mtokambali amesema kuwa Baraza hilo kupitia kwa madhehebu wanachama wake litaendelea kushirikiana na Serikali katika kuendeleza sekta za elimu, na afya nchini kwa kujenga na kuendesha mahospitali, vituo vya afya, mashule, vyuo vya aina mbalimbali.
“Hili sio tu kwamba linapunguza mzigo mkubwa wa Serikali katika kuihudumia jamii kubwa ya watanzania katika mahitaji husika, bali pia linasaidia kupunguza tatizo kubwa la ukosefu wa ajira kwa vijana.”

“Baraza limekuwa mstari wa mbele kupinga vitendo kama ndoa za jinsia moja, ushoga, kutokuwajibika kwa wazazi kutunza familia kunakopelekea kuongezeka kwa Watoto wa mitaani, mila potofu za ukeketaji wanawake, Imani za kishirikina zinazopelekea watu wenye ulemavu wa ualbino kuuawa kwa dhana”.