IRINGA-Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amezipongeza taasisi za dini likiwemo Kanisa Katoliki kwa kuendelea kushirikiana na Serikali katika kutoa huduma mbalimbali za kijamii kwa wananchi.
Amesema kuwa kitendo cha Kanisa Katoliki cha kuamua kuipandisha hadhi Hospitali ya Tosamaganga na kuwa Hospitali ya Rufaa kwa ngazi ya Mkoa ni cha kishujaa kwani kitaufaanya mkoa wa Iringa kuwa na hospitali mbili za rufaa na hatimaye kupunguza adha kwa wakazi wa mkoa huo kusafiri kwenda mikoa ya Dar es Salaam na Dodoma kufuata huduma za kibingwa.
Ametoa pongezi hizo leo Jumamosi, Julai 6, 2024) mara baada ya kuzindua hospitali ya rufaa ya Tosamaganga ngazi ya Mkoa pamoja na huduma za mionzi kwenye hospitali hiyo, iliyopo wilayani Iringa, mkoani Iringa.
Waziri Mkuu ambaye yuko mkoani Iringa kwa ziara ya kikazi ya siku nne, amesema kuwa uamuzi wa kuipandisha hadhi hospitali hiyo ni kuunga mkono jitihada za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya karibu na maeneo yao.
“Dhamira ya Rais Dkt. Samia ni kuwatumikia wananchi kwa kuhakikisha sekta ya afya inafika kila mahali ikiwemo kujenga hospitali kwenye kila Halmashauri. Watanzania endeleeni kuwa na imani Serikali yenu, nasi tutaendelea kuwahudumia ipasavyo.”
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali hiyo, Dkt. Benjamin Mfaume ameishukuru Serikali kwa misaada ya hali na mali inayotolewa kwenye hospitali hiyo ili kuiwezesha kutoa huduma bora kwa Watanzania.
“Katika mwaka 2022/2023, Serikali ilitoa shilingi bilioni 2.2 zikiwa ni mishahara ya wafanyakazi, dawa kupitia MSD na Basket Fund kupitia Halmashauri ya Wilaya ya Iringa na "OC" kupitia Serikali Kuu na hadi sasa Serikali bado inaendelea kufanya hivyo,” amesema.
Alisema hospitali hiyo, inahudumia wagonjwa kati ya 62,000 hadi 78,000 kwa mwaka ikiwa ni wastani wa wagonjwa 7,000 hadi 8,000 kwa mwezi huku idadi kubwa ikiwa ni ya akinamama wajawazito na watoto.