DODOMA-Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Deogratius Ndejembi amewataka Menejimenti na watumishi wa Wizara ya Ardhi kuondoa urasimu na kutoa hati milki za ardhi kwa wakati.
“Tuondoe urasimu, kama mtu ana nyaraka zote zinazohitajika, tuwape hati zao na tukumbuke sisi ni watoa huduma kwa wananchi n ani wizara wezeshi, hati zitolewe kwa wakati na hati zilizotayari wananchi wajulishwe waje wachukue hati zao,” amesema Mhe. Ndejembi.

Amewataka watendaji wa sekta ya ardhi nchini kufanya kazi kwa weledi na kusimamia vizuri mifumo ya TEHAMA na Mawasiliano ili wananchi wapate haki yao katika sekta ya ardhi.


Akimkaribisha Waziri Ndejembi kwenye kikao na Menejimenti ya Wizara hiyo, Naibu Waziri Geofrey Pinda amesema Wizara hiyo ina ofisi katika halmashauri zote nchini na kumhakikishia ushirikiano katika kutekeleza majukumu yake ili kuwahudumia wananchi katika Sekta ya Ardhi.
Awali Katibu Mkuu Mhandisi Anthony Sanga akimkaribisha Waziri wa Ardhi wizarani amemuelezea muundo wa wizara na kuainisha idara na vitengo vya wizara hiyo sambamba na taassisi zilizo chini ya wizara hiyo.