Waziri Simbachawene aipa tano TARURA kwa kufungua barabara kwenye milima mikali Kata ya Mang’aliza

DODOMA-Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora na Mbunge wa Kibakwe, Mhe. George Simbachawene ameishukuru na kuipongeza Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kwa kuanza kujenga barabara za zege kwenye milima mikali iliyopo Kata ya Mang’aliza-Kibakwe wilayani Mpwapwa. Waziri Simbachawene ametoa kauli hiyo wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa miundombinu inayosimamiwa na TARURA iliyofanywa na Naibu Katibu Mkuu wa OR-TAMISEMI anayeshughulikia miundombinu Mhandisi Rogatus Mativila.
“Niwashukuru sana TARURA kwa kutusaidia tulio kwenye mazingira magumu, jimbo langu la Kibakwe lipo katika maeneo tambarare na milimani, na hii ni milima mikali ambayo ipo karibu Kata sita na hakuna namna yoyote ya kutengeneza barabara zaidi ya barabara za zege.”

Ameongeza kusema kuwa utaratibu huo wa TARURA wa kujenga barabara za zege waliouanza miaka michache iliyopita umeanza kuleta ufanisi mkubwa hususan kufungua maendeleo pamoja na kuwaletea huduma nyingine wananchi ikiwemo umeme, shule ya sekondari pamoja na vituo vya afya.
“Kata ya Mang’aliza haikuwa na maendeleo kabisa lakini hii barabara ilivyofunguliwa hivi karibuni imeleta maendeleo kwa wananchi kwani miaka ya nyuma nilikuwa nakuja huku kwa pikipiki lakini sasa hivi nakuja kwa gari na hata magari makubwa yanafika kuleta vifaa vya ujenzi ambapo kuna shule ya sekondari inajengwa, kwasababu sehemu korofi zote zimewekwa zege, kwakweli nawapongeza sana TARURA,” amesema Mhe. Simbachawene.

Katika hatua nyingine, Mhe. Simbachawene ametumia fursa hiyo kuiomba TARURA kuendelea kutenga fedha kwa maeneo mengine ili kuhakikisha maeneo yote korofi yanawekwa zege ili kuchagiza huduma nyingine za kijamii.
‘‘Mang’aliza ya sasa sio ile ya mwaka 2010 ilikuwa haina barabara ya kuwapelekea umeme na huduma nyingine wananchi, Ila kusema ukweli TARURA wamejitahidi sana wamefungua barabara na zinapitika na shughuli za kijamii zinaendelea," alisisitiza.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news