NA CATHERINE SUNGURA
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene ameishukuru na kuipongeza Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kwa kuanza kujenga barabara za zege kwenye milima mikali iliyopo kata ya Mang’aliza-Kibakwe wilayani Mpwapwa.
Waziri Simbachawene ameyasema hayo wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa miundombinu inayosimamiwa na TARURA iliyofanywa na Naibu Katibu Mkuu wa OR-TAMISEMI anayeshughulikia miundombinu, Mhandisi Rogauts Mativila.

“Niwashukuru sana TARURA na kuwapongeza kwa kutusaidia tulio kwenye mazingira magumu, jimbo langu la Kibakwe lipo katika maeneo tambarare na milimani, na hii ni milima mikali ambayo ipo karibu kata sita na hakuna namna yoyote ya kutengeneza barabara zaidi ya barabara za zege.”
Ameongeza kusema kuwa utaratibu huo wa TARURA wa kujenga barabara za zege waliouanza miaka michache iliyopita umeanza kuleta ufanisi mkubwa hususani kufungua maendeleo pamoja na kuwaletea huduma nyingine wananchi ikiwemo umeme, shule ya sekondari pamoja na kituo cha afya.

“Kata ya Mang’aliza haikuwa na maendeleo kabisa lakini hii barabara ilivyofunguliwa hivi karibuni imeleta maendeleo kwa wananchi kwani miaka ya nyuma nilikuwa nakuja huku kwa pikipiki lakini sasa hivi nakuja kwa gari na hata magari makubwa yanafika kuleta vifaa vya ujenzi ambapo kuna shule ya sekondari inajengwa, kwasababu sehemu korofi zote wameweka zege, kwakweli nawapongeza TARURA.
“Hata hivyo ombi langu tu waendelee kutenga fedha kwa maeneo mengine kwani Ilani na sera yetu sasa ni kuwapelekea umeme na huduma nyingine wananchi lakini changamoto ilikuwa ni barabara ila kusema ukweli TARURA wamejitahidi sana kwani fedha zinazohitajika ni nyingi ila kwa hicho kidogo wamefungua hizo njia na zinapitika na shughuli za kijamii zinaendelea kama kawaida tumeanza kuona tunatokea mahali panapo pambazuka," alisisitiza.
Aidha, Waziri huyo alimpongeza Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuhangaika kutafuta rasilimali fedha, watendaji wa TARURA kwa kazi nzuri pamoja na TAMISEMI kwa usimamizi ambapo ana imani nia ya kufungua barabara zaidi itaendelea.


Mhandisi Mativila amesema kwamba wao kama OR-TAMISEMI wataendelea kuhakikisha mlima huo unaboreshwa na kupitika ßmuda wote na kuahidi kuendelea kutoa fedha zaidi ili wananchi waendelee kuzalisha mazao mbalimbali na kupatiwa huduma za kijamii ikiwemo shule na afya.