DODOMA-Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora na Mbunge wa Kibakwe, Mhe. George Simbachawene amekerwa na wananchi wanaoendesha shughuli za kilimo katika milima ya Kibakwe huku akihofia kama hatua za haraka hazitachukuliwa vyanzo vya maji vitakuwa hatarini kutoweka.
Mhe. Simbachawene ametoa kauli hiyo leo wakati akizungumza na wananchi kwa nyakati tofauti kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kijiji cha Lutarawe, Njiapanda na Kikuyu, Jimbo la Kibakwe, Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa mkoani Dodoma ambapo amesema vyanzo hivyo vya maji ni tegemeo pekee la wakazi wa jimbo hilo.
yana manufaa makubwa kwa watu wote ilhali mazao yanayolimwa katika milima hiyo ni kwa ajili ya manufaa watu wachache.
Amesema vyanzo hivyo vya maji ndio vyanzo pekee vinavyotegemewa lakini kasi ya ukataji miti inazidi kushamiri juu ya milima hiyo kwa ajili ya kilimo, hali inayotishia maisha ya watu wote kwa ajili ya maslahi ya watu wachache.
Kufuatia hatua hiyo Mhe. Simbachawene amewataka Madiwani kwa kushirikiana na viongozi wa vijiji kuzungumza na wanaolima juu ya milima hiyo na kama hawatawaelewa basi sheria kali zichukuliwe dhidi yao kwani wanahatarisha uhai wa wananchi wa Kibakwe na taifa kwa ujumla.
"Milima mingi imebaki vipara miti mingi imekatwa kwa ajili ya kilimo hali inayochangia wakati wa mvua maji kushuka kwa kasi kutoka milimani na kusababisha uhalibifu wa miundombinu ya barabara, hii sio sawa kabisa, nawaagiza viongozi chukueni hatua za haraka kwani mnawajua kwa majina wanaoyafanya hayo," amesisitiza Mhe. Simbachawene.
Kutokana na uharibifu huo, Mhe.Simbachawene amesema tatizo la maji katika jimbo hilo halitaisha hata kama Serikali itatoa fedha kwa vile vyanzo vya maji vinazidi kuharibiwa.
Mhe. Simbachawene amesema,juhudi anazozifanya za kuwaletea miradi ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa vituo vya afya, shule, barabara pamoja na umeme itakuwa haina maana kama vyanzo hivyo vitatoweka kwani maji ni uhai.