Waziri Simbachawene apiga marufuku Watumishi wa Umma kusumbuliwa kufuatilia taarifa za uhamisho

NA LUSUNGU HELELA

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene amepiga marufuku Watumishi wa Umma kusumbuliwa kufuatilia taarifa zao za kiutumishi wanapohamia kwenye kituo kipya cha kazi badala yake wafanye kazi zao kwani hilo sio jukumu lao bali ni wajibu wa waajiri. Mhe. Simbachawene ametoa kauli hiyo leo wakati akizungumza na watumishi na wananchi kwenye mkutano wa hadhara katika Kijiji cha Mlimo katika Kata ya Lufu, Jimbo la Kibakwe, Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa jijini Dodoma ambapo amesema suala la taarifa za Mtumishi ni jukumu la mwajiri.
Amesema,kitendo cha taarifa za watumishi kutohamishwa kumesababisha Watumishi hao kushindwa kupimwa kwenye mfumo wa e-tendaji kazi kwa vile kunakuwa hakuna taarifa za watumishi hao katika kituo kipya cha kazi na hivyo mwisho wake watumishi kusumbuliwa kufuatilia taarifa za kule walikotoka.

Kufuatia hatua hiyo, Mhe. Simbachawene amemuelekeza Katibu Mkuu- UTUMISHI kushirikiana na Mamlaka zingine zilikokasimiwa madaraka hayo ya kuhamisha Watumishi kuhakikisha Mtumishi pindi anapohama kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine asisumbuliwe kuhusu taarifa hizo.
Hivyo,Mhe. Simbachawene ametoa muda wa kuhamisha taarifa za watumishi waliohama kuwa ifikapo Agosti 15 mwaka huu taarifa za watumishi wote ziwe zimehamishwa na baada ya hapo hatua kali za kinidhamu zitachukuliwa kwa wote watakaoshindwa kutekeleza jukumu hilo.
Amesema,suala la kuhamisha taarifa za Mtumishi kutoka alikokuwa na kwenda kituo kipya cha kazi ni jukumu la Mkurugenzi au anayeongoza Taasisi wakishirikiana na Maafisa utumishi na kuongeza kuwa wanatakiwa kuhakikisha taarifa hizo zinahamishwa ndani ya mwezi mmoja ili watumishi waliohamishwa waendelee kufanya kazi zao kwa ufasaha.
"Utapimaje utendaji kazi wa mtumishi au kumpatia ruhusa mtumishi aliyepata dharula ilhali taarifa zake zipo sehemu nyingine, hii sio sawa, huko ni kuwatesa watumishi,"amehoji Mhe. Simbachawene.
Amesema,malalamiko ya kutohamishwa kwa taarifa za watumishi yamekuwa mengi kutoka kwa watumishi huku akiwataka watumishi wanapohama kutekeleza majukumu yao na hakuna atakayesumbuliwa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news