DODOMA-Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora na Mbunge wa Kibakwe, Mhe. George Simbachawene amewataka viongozi na wananchi kuzingatia sheria za nchi katika kutoa na kupokea huduma.

Mhe. Simbachawene amesema ili kuendeleza amani na kuepusha machafuko basi sheria za nchi ni lazima zizingatiwe na kila mtu awe kiongozi au mwananchi wa kawaida.
Amesema Tanzania imejengwa kwa misingi ya haki na usawa na ndio maana rasilimali za nchi zinagawanywa kwa usawa katika maeneo yote ya nchi ili kuchagiza utawala bora na ndio maana imeendelea kuwa kisiwa cha amani.
Amesema,Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu ameendelea kutekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi kwa kuzingatia utoaji wa haki na usawa kwa wananchi wote bila kujali mahali walipo.
Ameongeza kuwa katika Jimbo la Kibakwe analoliongoza miaka ya nyuma vijiji vingi havikuwa na huduma nyingi za kijamii ikiwemo shule na zahanati lakini kwa sasa huduma hizo zote zipo maeneo mengi na wananachi wanaendelea kuhudumiwa.
Katika hatua nyingine, Mhe. Simbachawene ametoa wito kwa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) pamoja na Wakala wa Umeme Vijijini (REA) kuhakikisha zinatoa kipaumbele cha huduma wanazozitoa kwa Taasisi za kijamii zilizopo katika Kata ya Pwaga.
Amesema huduma muhimu kama vile umeme na barabara ni muhimu zikafikishwa haraka katika maeneo ya shule, makanisa, misikiti pamoja na ofisi za vijiji.

Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Pwaga, Mhe. Wilfred Mgonela ametumia fursa hiyo kumshukuru Mhe. Simbachawene kwa ushirikiano ambao ameendelea kumpa katika kuhakikisha miradi ya maendeleo inaendelea kutekelezwa katika Kata anayoiongoza huku akiwaomba wananchi kuendelea kushirikiana naye ili kujiletea maendeleo ya mtu mmoja mmoja na Kata kwa ujumla.