DODOMA-Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora na Mbunge wa Kibakwe, Mhe. George Simbachawene amewataka wananchi wa Kibakwe kuendesha kilimo cha biashara kwa kutumia miundombinu ya umeme iliyopo huku akiwaahidi kuwaletea mradi mkubwa wa kimkakati wa umwagiliaji.


Amesema,awali changamoto kubwa ilikuwa ni kilimo cha umwagiliaji cha kutumia nishati ya dizeli na petroli ambapo ilikuwa ni ngumu kuona tija kutokana na gharama kubwa ya nishati hiyo.
Ameongeza kuwa, umwagiliaji umekuwa duni kutokana na mifereji inayotumika kuwa ni ya kizamani na inachangia upotevu mkubwa wa maji.
"Tunataka mabadiliko makubwa katika jimbo letu, tunatamani kuona umeme tulionao unatupeleka mashambani na sio kuutumia tu kwa ajili ya kuwashia taa pekee majumbani mwetu," amesema Mhe. Simbachawene.
Amesema,umeme huo utumike kusukuma maji ya kumwagilia usiku na mchana katika mashamba ya wananchi huku akisema miaka 10 ijayo anaviona vijiji hivyo vikiwa katika viwango vya juu kiuchumi.

Kijiji cha Idodoma na Malolo ni miongoni mwa vijiji katika Jimbo la Kibakwe vinavyosifika kwa kustawisha zaidi kilimo cha vitunguu na maharagwe ambapo uhitaji wa mazao hayo umekuwa mkubwa ndani na nje ya nchi.