PRETORIA-Katibu Mkuu Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia, Prof. Carolyne Nombo na wataalamu wa elimu kutoka Tanzania Bara na Zanzibar wameshiriki kikao cha pamoja na Wizara ya ElimuMsingi ya Afrika Kusini ambapo ameipongeza wizara hiyo kwa jitihada kubwa wanazozifanya katika sekta ya elimu.

Prof. Nombo ameongeza kuwa Tanzania katika masuala hayo imejifunza na kwamba serikali itaona namna ya kuimarisha eneo hilo ili kuongeza ufanisi wa ufundishaji, ujifunzaji na upimaji wa wanafunzi shuleni.
Aidha, Prof. Nombo ameiahidi Afrika Kusini kuipatia msaada wa kitaalamu kutoka Tanzania katika tathmini ya mtaala na vifaa vyake kwa ajili ya kufundishia somo la Kiswahili katika shule nchini humo.
Sambamba na hilo, alitoa vitabu mbalimbali vya Kiswahili zikiwemo Kamusi, vitabu vya kufundishia Kiswahili kwa wageni, mitaala, mihutasari ya somo pamoja na vitabu vya taarifa za tathmini ya ufaulu wa watahiniwa kwa somo la Kiswahili.
Katibu Mkuu amesema, utoaji wa vitabu hivyo ni hatua za awali za kuchochea ufundishaji na ubidhaishaji wa lugha ya Kiswahili nchini humo.