Wizara ya Elimu yaweka jiwe la msingi ujenzi Chuo cha Ufundi cha Arusha kampasi ya Kikuletwa wilayani Hai

KILIMANJARO-Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imeweka Jiwe la Msingi la ujenzi wa Chuo Ufundi cha Arusha Kampasi ya Kikuletwa iliyopo wilayani Hai Mkoani Kilimanjaro kitakachokuwa Kituo cha Umahiri katika kutoa Nishati Jadidifu.
Akizungumza Julai 30, 2024 baada ya kuweka Jiwe hilo la Msingi Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda amesema kuwa Kituo cha Kikuletwa ni miongoni mwa vituo vinne vya umahiri vya kikanda vinavyojengwa na Serikali kwa kushirikiana na Benki ya Dunia.
Waziri Mkenda amesema kuwa Vituo hivyo vinajengwa kwa gharama ya Dola za Kimarekani milioni 75 sawa na takribani shilingi Bilioni 187.5 kupitia mradi ujulikanao kama East Africa Skills for Transformation and Regional Integration Project (EASTRIP) ambapo Chuo cha Ufundi Arusha kilipatiwa kiasi cha Dola za Kimarekani milioni 16.25 sawa na takribani Bilioni 37.5

Prof. Mkenda ameongeza kuwa Ujenzi wa Kituo hicho ni utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (2021/22 – 2025/2026) na kwamba ni muhimu kwani kitazalisha nguvukazi yenye ujuzi wa kutosha itakayosaidia uendeshaji wa miradi ya kimkakati ya Kitaifa hususan katika uzalishaji wa nishati kama vile ujenzi wa Mtambo ya Kuzalisha Umeme wa Bwawa la Mwalimu Nyerere.
"Mwelekeo wa Dunia sasa hivi ni kuhakikisha kwamba tunatumia nishati safi na endelevu bila kuharibu mazingira, hivyo kituo ni muhimu sana na kinaendana na azma ya Rais wetu Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwamba tuwe na nishati safi kwa ajili ya matumizi ya kupikia na mengine ni hatua kubwa katika mwelekeo wa Dunia ya kulinda tabia nchi kwa kuhakikisha kwamba hatuchomi mafuta kama dizeli yanayokwenda kuharibu hali ya hewa,” amesema Prof. Mkenda

Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Carolyne Nombo amesema kuwa Mradi wa Kujenga na Kuimarisha Ushirikiano wa Kikanda wa Afrika Mashariki (EASTRIP) ni muhimu kwa kuwa una kwenda kusaidia katika utekelezaji wa mabadiliko ya kielimu ambayo yameaanza kutekelezwa kupitia Sera ya Elimu na Mafunzo ya 2014, Toleo la 2023 pamoja na Mitaala mipya katika ngazi mbalimbali.
Prof. Nombo ameongeza kuwa Mradi huo umeshirikisha nchi tatu za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jamhuri ya Kenya na Shirikisho la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Ethiopia ambazo kwa ujumla zinatekeleza mradi kwa kuanzisha vituo vya umahiri kumi na sita (16).

Amesema kuwa, Tanzania ina vituo vinne vya Umahiri vya Chuo cha Ufundi Arusha (ATC) Kituo cha Umahiri cha Kikanda katika Mafunzo ya Nishati Jadidifu, Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) kinaanzisha kituo cha umahiri cha Kikanda katika mafunzo ya Usafirishaji wa Anga na Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam ambacho kina Vituo viwili vya Umahiri ambavyo ni Kituo cha Umahiri cha Kikanda katika Tehama kupitia Kampasi ya Dar es Salaam na kituo cha Umahiri cha Kikanda katika Teknolojia ya Ngozi katika Kampsi ya Mwanza.
Mkuu wa Wilaya ya Hai, Mhe. Amiri Mkalipa akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro ameishukuru Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa kujenga Kampasi hiyo katika wilaya ya Hai ambayo itakwenda kuinua Uchumi wa wana Hai na Kijiji cha Cheemka kwa kuwa kuna uzalishaji wa mazao ya vyakula ambayo yatatumika katika kulisha wanachuo wa kampasi hiyo.
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Hai Wanguba Maganda ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa kuwatumika wananchi wa Kilimanjaro na Hai kwa kuwapatia Chuo Kikubwa na kuwataka wananchi hao kuonyesha uzalendo kwa kuitunza na kuilinda Kampasi hiyo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news