Wizara ya Madini yaendesha Kliniki ya Madini mkoani Songwe

SONGWE-Naibu Waziri wa Madini Mhe. Dkt. Steven Kiruswa leo Julai 3, 2024 amekutana na wachimbaji wadogo, wachenjuaji na wafanyabiashara wa madini Mkoa wa Songwe na kupokea changamoto mbalimbali zinazowakabili katika maeneo yao ya kazi.
Akizungumza katika mkutano huo ambao umefanyika katika kijiji cha Saza Wilayani Songwe, Dkt. Kiruswa amesema kuwa Wizara ya Madini na taasisi zake imeanzisha kliniki ya madini kwa wachimbaji wa madini nchini kwa lengo la kutatua changamoto zinazowakabili wachimbaji ndani ya sekta pamoja na sekta zinazofungamana na sekta ya madini ikiwemo sekta ya nishati.
Dkt. Kiruswa amefafanua kuwa, Serikali inatambua mchango wa wachimbaji wadogo katika Pato la Taifa hivyo ipo kila sababu ya kufahamu changamoto zinazowakabili na kutengeneza mkakati endelevu wa kuzitatua kwa kushirikiana na sekta zinazofungamana na sekta ya madini.
Awali, akielezea hali ya uzalishaji wa madini ya dhahabu kutoka kwa wachimbaji wadogo na wachenjuaji, Afisa Madini Mkazi Mkoa wa Songwe Chone Malembo, amesema kuanzia Julai 2023 mpaka Julai 2024 kiasi cha kilogramu 1,059.35 zimezalishwa kutoka kwa wachimbaji wadogo.

Akielezea kuhusu mkakati uliopo, Malembo ameeleza kuwa ofisi inaendelea kubainisha maeneo yaliyo wazi na kuangalia leseni za utafiti ambazo hazifanyiwa kazi ili kutoa mapendekezo maeneo yanayofaa kuwapatia wachimbaji wadogo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Wachimbaji Wadogo wa Madini Mkoani Songwe (SOREMA), Emmanuel Kamaka amebainisha changamoto zinazowakabili wachimbaji ikiwa pamoja na ukosefu wa nishati ya umeme ya uhakika, utitiri wa kodi katika mnyororo mzima wa madini , utoaji wa leseni katika maeneo yanayofanyiwa kazi kwa pamoja zinasababisha uchimbaji kuwa mgumu.
Kuanza kwa Kliniki ni sehemu ya utekelezaji wa maazimio yaliyotolewa wakati wa mkutano mkuu wa mwaka 2024 wa Shirikisho la Wachimbaji Wadogo wa Madini Tanzania (FEMATA) ambapo kliniki hiyo imejumuhisha wataalam kutoka taasisi mbalimbali za Umma ikiwemo TANESCO, GST, STAMICO, NEMC, TRA, Mkemia Mkuu wa Serikali na Halmashauri ya Wilaya ya Songwe.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news