DODOMA-Wizara ya Madini imekutana na Kampuni ya Prediction Software Incorporated kutoka Nchini Marekani na kujadili mfumo bora wa kuboresha biashara ya madini hapa nchini kwa njia ya kidijitali na teknolojia ya kisasa.
Kikao hicho kimefanyika leo Julai 24, 2024 katika Ofisi za Wizara ya Madini zilizopo Mji wa Serikali Mtumba Jijini Dodoma, ambapo Rais wa Prediction Software Inc., Gene Chandler, amewasilisha mfumo wa kiteknolojia wa kufuatilia na kudhibiti biashara ya madini ya Metali yakiweno Dhahabu (The Mineral Trading Management System – Gold Tracker).

Katika wasilisho hilo, Gene Chandler ameeleza kuwa mfumo huo wa kidijitali unalenga kutatua changamoto mbalimbali zinazokabili Sekta ya Madini hususan katika ufuatiliaji, udhibiti, na utoaji sahihi wa hesabu.
“Mfumo huu unahusisha utoaji leseni, ukusanyaji wa mirabaha, tozo, na biashara ya Madini ya Metali kama Dhahabu. Kwa kutumia The Gold Tracker na XRF Precious Metal Analyzers, wateja wanaweza kuongeza mapato yao kupitia ukusanyaji sahihi na wa haraka wa ushuru na kodi, huku pia wakilinda mazingira na rasilimali za nchi kupitia usimamizi bora wa leseni” amesema Chandler.
Chandler ameendelea kueleza kuwa teknolojia hii tayari imeshatumika katika nchi kadhaa, ikiwemo Marekani, Canada, Australia, na Afrika ya Kusini imeonyesha mafanikio makubwa katika kuboresha usimamizi na biashara ya madini.
Amesisitiza umuhimu wa Tanzania kuzingatia matumizi ya teknolojia hii ili kufikia viwango vya kimataifa katika sekta ya madini.

Dkt. Mwanga amesema kuwa wataalam wa Wizara watakaa na kujadili kwa kina kuhusu mfumo huo wa teknolojia ya kisasa uliowasilishwa na Prediction Software Inc., na kwamba lengo ni kuona jinsi mfumo huo unavyoweza kutumika kwa ufanisi nchini Tanzania ili kuboresha usimamizi wa madini na kuongeza mapato ya Serikali.



Hatua hiyo ni muhimu katika juhudi za Serikali kuboresha usimamizi na biashara ya madini nchini kwa kutumia teknolojia ya kisasa.