WTTC yatabiri matokeo makubwa Sekta ya Utalii Tanzania, matarajio ni kuchangia robo tatu ya Bajeti Kuu ya Serikali

LONDON-Sekta ya Utalii Tanzania inatarajiwa kuchangia robo tatu ya Bajeti Kuu ya Serikali ya sasa ifikapo mwaka 2034.
Hayo ni kwa mujibu wa ripoti mpya ya Baraza la Utalii Duniani (Travel & Tourism Council,WTTC) iitwayo Travel and Tourism: Economic Impact Research 2024.

Ni ripoti iliyotolewa Juni 26, 2024 jijini London nchini Uingereza ambayo inaonesha Tanzania kuwa, moja ya mataifa ambayo yameendelea kunufaika kiuchumi na mageuzi makubwa yanayoendelea nchini chini ya Rais wa Awamu ya Sita, Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Sekta ya Utalii.
Kwa ujumla ripoti hiyo imebainisha kuwa, utalii na safari viliingizia Tanzania shilingi trilioni 18.6 mwaka jana 2023, ikiwa ni rekodi kubwa ya mapato kuwahi kutokea ikizidi ile ya mwaka 2019 (kabla ya Uviko-19) kwa nyongeza ya asilimia nne.
Aidha,kiasi kilichotumiwa na watalii kwa huduma mbalimbali (visitor spending levels) kimepanda mwaka jana 2023 na kuweka rekodi ya juu zaidi ambapo watalii wa nje walitumia shilingi trilioni 8 huku wa ndani wakitumia shilingi trilioni 3.7 sawa na ongezeko la asilimia 11.1 na 12.8 mtawalia ikilinganishwa na mwaka 2019.


Ripoti hiyo pia inaonesha kuwa, ajira katika sekta ya utalii Tanzania mwaka 2023 zilifikia watu milioni 1.4 ikiwa ni ongezeko la ajira 97,000 lakini zikiwa pungufu kidogo kwa asilimia 7.4 ikilinganishwa na rekodi ya juu mwaka 2019.
Wakati huo huo,kwa mwaka 2024 matarajio ya mchango wa sekta ya utalii nchini, taarifa hiyo ya WTTC inaeleza kuwa ni kufikia shilingi Trilioni 20.4 na kukua hadi shilingi Trilioni 31 katika miaka kumi ijayo (kiwango ambacho ni takribani robo tatu ya Bajeti ya sasa ya Serikali ya shilingi Trilioni 49) huku ajira zikitarajiwa kuweka rekodi mpya na ya juu zaidi kuwahi kutokea nchini kwa mwaka huu kufikia zaidi ya ajira milioni 1.5.

“Sekta ya Utalii ya Tanzania inazidi kuimarika kila uchao ikiweka rekodi za juu kuwahi kufikiwa,” anasema Mtendaji Mkuu wa WTTC Julia Simpson kuhusu ripoti ya Tanzania. Aidha, Tanzania ni miongoni mwa nchi chache za Afrika ambazo mafanikio yake yamechambuliwa kwa kina katika tovuti ya baraza hilo. Soma hapa》》》

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news