Yanga SC yatwaa Toyota Cup, yamdhalilisha Nasreddine Nabi kwa mabao 4-0

NA GODFREY NNKO

WAKATI mashabiki wa Young Africans Sports Club (Yanga SC) ya jijini Dar es Salaam wakiimalizia wikiendi yao kwa raha mustarehe upande wa Kaizer Chiefs mambo ni magumu.

Ugumu huo unakuja baada ya vijana hao wa Soweto kutundikwa mabao 4-0 ndani ya Toyota Stadium uliopo Bloemfontein nchini Afrika Kusini.
Ushindi huo umedhirisha kuwa, vijana wa Kocha Mkuu Miguel Gamondi wameupania vilivyo msimu mpya wa 2024/25 wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara.

Pengine swali linaweza kuwa, vijana hao wa Soweto kichapo hiki kinamaanisha nini licha ya mabadiliko yaliyofanywa na uongozi wa klabu hiyo?.

Jibu linaweza kuwa ni suala la muda na subira, kwani matokeo hasi msimu uliopita yalisababisha mabadiliko katika benchi la ufundi. Benchi lenyewe linaongozwa na Nasreddine Nabi.

Ikumbukwe Mwalimu Nabi awali aliwanoa Yanga na kabla ya kukutana nao leo Julai 28,2024 amekuwa na vijana hao wa Soweto kwa wiki tatu nchini Uturuki, akijaribu kukiweka kikosi chake imara.

Kaizer Chiefs katika michezo yao miwili ya mwisho ya kujiandaa na msimu mpya, kabla ya mechi dhidi ya Yanga walipata ushindi wa mabao 5-2 dhidi ya Al Shahaniya ikiwa ni kabla ya kucheza sare ya bila kufungana na Dibba Al-Hisn.
Ni matokeo yaliyowapa matumaini mashabiki wa Kaizer Chiefs na walitarajia pengine leo wangeionesha ubabe Yanga SC, lakini mambo yakawa magumu.

Yanga SC ambayo ilikuwa imeifunga TS Galaxy kwa mchezo wa pekee Jumatano, haikuwa tayari kuonesha udhaifu.

Jumatano bao la Yanga lilifungwa na Prince Dube dkika ya 55 kupitia mechi iliyopigwa uwanja wa Kanyamazane uliopo mji mdogo wa Kanyamazane katika jimbo la Mpumalanga nchini Afrika Kusini.

Aidha, mchezo wa leo mchezaji huyo wa Kimataifa wa Zimbabwe, Prince Dube ndiye aliyewafungulia waajiri wake Yanga pazia la ushindi.

Ni baada ya kutundika bao safi dakika ya 25 ya kipindi cha kwanza ambalo liliwatibua Kaizer Chiefs ingawa hasira zao hazikuweza kuzaa matunda.

Mabao mengine yalifungwa na Aziz Ki mawili dakika ya 45' na 63 huku Clement Mzize akipachika moja dakika ya 57.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news