JOHANNESBURG-Serikali ya Afrika Kusini imewafukuza raia 95 wa Libya ambao walikamatwa mwezi uliopita katika kambi ya siri inayodhaniwa ni ya kijeshi katika Jimbo la Kaskazini Mashariki mwa Mpumalanga nchini humo.
Picha na Zimlive.
Uamuzi huo umefikiwa Agosti 18,2024 ambapo Waziri wa Mambo ya Ndani wa Afrika Kusini, Leon Schreiber amesema, wizara yake itaendelea kutumia uwezo wake kuhakikisha sheria za uhamiaji zinaheshimiwa kote Afrika Kusini.
Inadaiwa raia hao wa Libya waliingia Afrika Kusini mwezi Aprili kwa vibali vya kusoma ili kuwa walinzi, na walikamatwa mwezi Julai, mwaka huu wakati wa msako wa polisi kwenye kambi ya mafunzo ya kijeshi katika mji wa White River huko Mpumalanga.
Kwa mujibu wa Jeshi la Afrika Kusini, vilipatikana vifaa vya mafunzo ya kijeshi na dawa za kulevya kwenye kambi hiyo.
Raia hao wa Libya wanadaiwa kupokea mafunzo ya kijeshi kinyume cha sheria, kukiuka masharti ya Visa zao na Sheria ya Uhamiaji nchini humo.(AP/NA).