NA DIRAMAKINI
MATAJIRI wa Dar es Salaam, Azam FC wametwaa alama tatu zikisindikizwa na bao moja baada ya kutembeza kichapo kwa APR FC ya Rwanda.
Ni katika mchezo wa mkondo wa kwanza wa hatua ya awali ya kuwania kufuzu Ligi ya Mabingwa barani Afrika msimu wa 2024/25.
Mtanange huo umepigwa leo Agosti 18,2024 katika dimba la Azam Complex lililopo Kata ya Chamazi ndani ya Halmashauri ya Manispaa ya Temeke jijini Dar Es Salaam.
Penati ya kipindi cha pili ya Jhonier Blanco dakika ya 55' ilitosha kuipa Azam FC ushindi wa bao 1-0 dhidi ya APR.
Aidha,mchezo wa marudiano utapigwa Agosti 25, 2024 katika dimba la Taifa la Amahoro jijini Kigali nchini Rwanda ambao utaamua timu itakayokata tiketi ya hatua ya kwanza.
Kwa matokeo hayo, Azam FC imepokea shilingi milioni 5 za hamasa kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Dkt.Samia Suluhu Hassan.