LINDI-Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Balozi Dkt.Emmanuel Nchimbi amepokea taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi katika Jimbo la Mchinga mkoani Lindi huku alimpongeza Mbunge wa jimbo hilo, Mama Salma Kikwete kwa kazi nzuri.
"Niseme nimeisikiliza taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM, tena kwa umakini sana kwa niaba ya CCM nakupongeza wewe na viongozi wenzako kwa kazi kubwa unayofanya. Umetembelea kata zote na vijiji vyote.
"Umetumia hadi bodaboda na bajaji kuwafikia wananchi wa Jimbo la Mchinga, unaguswa na changamoto za wananchi wenzako wa Mchinga na unapambana kutatua kero zao kwa kuzisemea Bungeni na kuwaomba mawaziri kufika huku wao wenyewe.”
“Wakati wanatazama ile video ya uwasilishaji wa taarifa hiyo ya utekelezaji wa ilani, kuna mama mmoja amesema hakutegemea kwa hadhi yako ulivyo, kwamba ungeweza kulizunguka jimbo zima la Mchinga.
"Mimi pamoja na wenzangu Wajumbe wa Sekretarieti tumefurahishwa sana ya utekelezaji huu mzuri wa Ilani ya CCM ya Uchaguzi 2020/2025, ndani ya miaka hii mitatu. Tunakutakia kila la heri katika kumalizia hayo mengine yaliyobakia katika kukamilisha Ilani ya 2020 - 2025.”

Baada ya kuwasilisha taarifa hiyo Julai 31,2024, Mama Salma Kikwete amekabidhi pikipiki kwa Polisi Jamii wa Jimbo la Mchinga na shule za sekondari katika kata zote za jimbo hilo.