Balozi Nchimbi awaita Mambo ya Ndani ziara yake kujibu masuala ya NIDA

KAGERA-Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi amemwagiza Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi ama Naibu Waziri wake, kuungana nae ziarani Kagera kwa ajili ya kuyatolea ufafanuzi malalamiko ya wananchi yanayohusu upatikanaji wa Vitambulisho vya Uraia vinavyotolewa na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA).

Balozi Nchimbi ambaye yuko katika ziara yake ya siku 6 mkoani Kagera, ametolea maelekezo hayo aliposimama kuwasalimia wananchi wa Kyerwa, katika Uwanja wa Nkwenda Maziwa, akiwa njiani kuelekea Karagwe leo Agosti 8, 2024.
“Tangu nimeanza ziara maeneo ya Mkoa wa Kigoma na hapa Mkoa wa Kagera wananchi wanalalamikia upatikanaji wa Vitambulisho vya NIDA. Hapa pia ninyi kupitia kwa Mbunge wenu Innocent Bilakwate mmelilalamikia.

“Nimeshatolea maagizo mahali pengine mchakato wa upatikanaji wa vitambulisho vya NIDA uboreshwe na uharakishwe ili wananchi wapate utambulisho wao. Na nimesema wananchi kudai vitambulisho ni dalili ya mapenzi kwa nchi yao.

“Lakini kupitia mkutano huu, naomba kumwelekeza Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi au Naibu Waziri wake, aungane nasi awe sehemu ya msafara wa ziara yangu ili atolee ufafanuzi malalamiko ya wananchi kuhusu Vitambulisho vya Uraia,” amesema Balozi Nchimbi.

Katika ziara hiyo, yenye malengo ya kukagua utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM, kuhamasisha uhai wa chama na kuwasikiliza wananchi, Katibu Mkuu wa CCM Balozi Nchimbi ameambatana na Ndugu Issa Haji Usi Gavu, Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC) - Oganaizesheni, Ndugu Amos Gabriel Makalla, Katibu wa NEC - Itikadi, Uenezi na Mafunzo na Ndugu Rabia Abdalla Hamid, Katibu wa NEC - Siasa na Uhusiano wa Kimataifa, ambapo leo atakuwa Wilaya za Kyerwa na Karagwe.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news