Biashara na sekta hizi zinaweza kuathirika mvua za vuli-TMA

NA GODFREY NNKO

KAIMU Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) na Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi, Dkt. Ladislaus Chang’a amesema, kuelekea msimu wa mvua za Vuli mwezi Oktoba hadi Desemba,2024 kuna uwezekano shughuli za kibiashara zinazohusisha hali ya hewa zikaathirika.
Ameyasema hayo leo Agosti 22,2024 jijini Dar es Salaam wakati akiwasilisha taarifa mbele ya wanahabari kuelekea mvua za Vuli mwaka huu.

"Shughuli za kibiashara zinazohusisha hali ya hewa zinaweza kuathirika kutokana na kuongezeka kwa gharama za uzalishaji kutokana na matumizi makubwa ya nishati katika uhifadhi wa mazao tete na bidhaa."

Dkt.Chang'a amesema,mvua za chini ya wastani zinaweza kusababisha kuathirika kwa ubora wa miti ya nguzo na mbao.

"Wadau wa sekta binafsi wanashauriwa kushirikiana na wataalam mbalimbali ikiwemo wataalam wa hali ya hewa ili kukabiliana na athari zinazoweza kujitokeza.


"Hatua za kupunguza matawi ya miti ya nguzo na mbao zitekelezwe mara kwa mara. Taasisi za benki na bima zinashauriwa kuandaa na kutoa huduma mahususi kwa wadau ili kujenga ustahimilivu katika biashara."

Wakati huo huo, Dkt.Ladislaus Chang’a amesema,kupungua kwa kina cha maji katika mito, mabwawa na hifadhi ya maji ardhini kunatarajiwa kujitokeza hususani katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za chini ya wastani.

"Hali hii inaweza kupunguza upatikanaji wa maji kwa matumizi mbalimbali. Uzalishaji wa madini hususani dhahabu kwa wachimbaji wadogo na nishati ya umeme utokanao na maji unaweza kuathirika (unaweza kupungua)."

Amesema, katika sekta ya maji, watumiaji wanaweza kuathirika kijamii, kiuchumi, na mazingira na kupelekea migogoro kati ya watumiaji wakubwa na wadogo.

Hata hivyo, amesema utekelezaji wa miradi ya miundombinu ya maji, umeme, utafutaji na
uchimbaji wa mafuta na gesi unatarajiwa kuendelea vizuri.

"Wadau wanasisitizwa kuzingatia mgawanyo wa maji na matumizi endelevu ya maji katika shughuli za kuchakata madini, uzalishaji wa umeme, matumizi viwandani na majumbani.

"Vile vile, mamlaka husika zinashauriwa kuwa na mipango madhubuti ya matumizi ya vyanzo mbadala vya nishati."

Kwa kuzingatia mvua za chini ya wastani zinazotarajiwa katika msimu wa Vuli, Dkt.Ladislaus Chang’a amesema,mamlaka za miji zinashauriwa kuongeza uelewa kwa Timu ya Menejimenti ya Halmashauri (CMT).

Sambamba na madiwani ili kuendeleza mipango na bajeti kwa ajili ya maandalizi ya msimu katika sekta zinazotarajiwa kuathirika.

"Mamlaka za miji zinashauriwa kuhakikisha kuwa wadau wanaotoa huduma wanaratibiwa na kutoa taarifa za tahadhari za mapema zinazoshughulikia sekta mbalimbali.

"Kwa upande mwingine, mamlaka zinahimizwa kuchukua hatua madhubuti ili kuboresha mifumo ya usambazaji wa maji safi na taka."

Amesema,licha ya upungufu wa mvua kwa jumla, vipindi vifupi vya mvua kubwa vinatarajiwa, na hivyo kuhitaji maandalizi.

Dkt.Chang’a amesema, mamlaka za miji zinashauriwa kuhakikisha njia zote zinapitika vizuri kwa wakati wote na miundombinu iboreshwe ili kupunguza maji kujaa katika mifereji na mitaa.

Vile vile amesema, hali ya upungufu wa upatikanaji wa maji safi na salama inaweza kujitokeza na kusababisha magojwa ya mlipuko katika maeneo husika.

Miongoni mwa magonjwa hayo ni vikope, magonjwa ya ngozi, kipindupindu na homa ya matumbo, changamoto za kupumua na magonjwa yanayohusiana na joto kali.

"Mamlaka husika zinashauriwa kuchukua hatua stahiki ili kupunguza athari hasi, ikiwa ni pamoja na kuhimiza wananchi kutibu maji kabla ya kunywa, kusafisha matunda, kunywa maji safi, salama na ya kutosha.

"Ni ili kuepuka upungufu wa maji mwilini sambamba na kuzingatia usafi wa mwili na mazingira. Pamoja na hayo, mamlaka husika zinasisitizwa kutoa elimu ya afya kwa jamii ikiwemo kuzingatia usafi binafsi, matumizi ya maji safi na salama pamoja na usafi wa mazingira yanayowazunguka."


Dkt.Chang’a amesema, upungufu wa mvua unaotarajiwa katika msimu huu unaweza kuleta madhara ya upatikanaji wa chakula, malisho ya mifugo na maji.

Amesema,mamlaka husika zinashauriwa kushirikiana na kuhakikisha uwepo wa usalama wa chakula, malisho ya mifugo, maji na kutoa miongozo ya namna ya kukabiliana na maafa ili kuzuia na kupunguza athari zinazoweza kujitokeza.

"Hivyo, mamlaka husika na Kamati za Usimamizi wa Maafa katika ngazi za mikoa, wilaya, kata na vijiji zinashauriwa kushirikiana na kuchukua hatua za kuzuia, kujiandaa na kukabiliana na maafa ikiwemo kutoa elimu na miongozo itakayohamasisha kilimo cha mazao yanayostahimili ukame, uhifadhi wa chakula, maji na malisho ya mifugo,"amesisitiza Dkt.Ladislaus Chang’a.

Msimu wa mvua za vuli mahususi zitakuwa maeneo ya Nyanda za Juu Kaskazini Mashariki ikijumuisha mikoa ya Arusha, Manyara, na Kilimanjaro, Pwani ya Kaskazini, Kaskazini ya Mkoa wa Morogoro.

Mikoa ya Pwani ikijumuisha Visiwa vya Mafia, Dar es salaam, Tanga na mikoa ya Ukanda wa Ziwa Victoria.

Dkt.Chang’a amebainisha kuwa, Kanda ya Ziwa Victoria mvua za mvuli zinatarajiwa kuwa wastani hadi chini ya wastani katika maeneo mengi ambapo zitaanza wiki ya nne ya mwezi Septemba, 2024 katika mikoa ya Geita.

Kagera na Kaskazini mwa Mkoa wa Kigoma na kutawanyika maeneo mengine katika wiki ya kwanza na ya pili ya mwezi Oktoba, 2024.

Amesema kuwa,mvua hizo zinatarajiwa kuisha wiki ya tatu na ya nne ya mwezi Desemba, 2024.

Vile vile amesema, mvua za vuli za wastani maeneo ya Pwani, Morogoro, Visiwa vya Mafia, Dar es Salaam, Tanga na Visiwa vya Unguja na Pemba zinatarajiwa kuanza wiki ya pili na ya tatu ya mwezi Oktoba, 2024 na kuisha wiki ya nne ya mwezi Desemba, 2024.

Aidha, Nyanda za Juu Kaskazini Mashariki ambayo ni mikoa ya Arusha, Manyara na Kilimanjaro kutakuwa na mvua za wastani hadi chini ya wastani kuanzia wiki ya tatu ya mwezi Oktoba, 2024 na kuisha wiki ya nne ya mwezi Desemba, 2024.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news