DODOMA-Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali Tanzania (SHIMIWI) limesema Bonanza la uzinduzi wa michuano ya
SHIMIWI mwaka 2024 linafanyika leo Agosti 10, 2024 katika Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma.
Ikiwa ni maandalizi kwa timu za watumishi wa umma wanaofanya kazi katika Wizara na Idara za Serikali Tanzania Bara kuelekea michezo ya SHIMIWI itayofanyika kuanzia Septemba 18,2024 mkoani Morogoro.
Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu wa Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali Tanzania (SHIMIWI),Alex Temba.
Amesema, mgeni rasmi katika Bonanza hilo anatarajiwa kuwa Katibu Mkuu Kiongozi, Bal-
ozi Dkt. Moses Kusiluka ambaye ni mlezi wa shirikisho hilo.
Kaulimbiu ya mwaka 2024 inasema" Michezo Huboresha Utendaji Kazi, Shiriki Uchaguzi wa
Serikali za Mitaa kwa Ujenzi wa Taifa Endelevu".
Bonanza hilo litatanguliwa na mbio fupifupi (jogging) zitakazoanzia viwanja vya Bungena
kumalizikia kwenye uwanja wa Jamhuri Jijini Dodoma ambako kutakuwa na michezo mbalimbali ikiwemo Mpira wa Miguu, Netiboli, pamoja na mchezo wa kuvutana kwa kamba Wanaume na Wanawake.
Michuano ya SHIMIWI ni miongoni mwa mashindano makubwa yenye kushirikisha watumishi wa umma takribani 3000 kwa wakati mmoja.
Temba amesema, yamekuwa ni mashindano yenye hamasa kubwa na timu zinaongezeka kila mwaka kutokana na maelekezo yanayotolewa na viongozi wa Kitaifa mara kwa
mara yakihamasisha watumishi kufanya mazoezi ili kuwa na afya njema itakayowawezesha kutoa huduma bora kwa wananchi.
"Takwimu katika mwaka 2021 zinaonesha vilabu 47 vilishiriki, mwaka 2022 vilabu 62 na mwaka 2023 vilabu 74 hivyo nina imani kubwa kwamba mwaka huu 2024 vilabu vingi zaidi
vitashiriki."