ZANZIBAR-Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi amewahimiza wanachama wa CCM kujiandikisha kwa wingi katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura mwezi Januari, mwakani.
Ni ili kuwa na sifa ya kushiriki Uchaguzi Mkuu na kukihakikishia Chama Cha Mapinduzi ushindi wa kishindo kutokana na wingi wa wanachama wa CCM kupitia jumuiya zake.
Dkt.Mwinyi amesema hayo Agosti 22,2024 alipozungumza na Wajumbe wa Kamati za Siasa za Halmashauri Kuu ya CCM ngazi ya Matawi, Wadi, Jimbo, Wilaya, na Mkoa katika viwanja vya Tibirinzi, Mkoa wa Kusini Pemba.

Aidha, Dkt. Mwinyi ameahidi kujibu kwa takwimu sahihi hoja zote zinazopotoshwa, hakuna jambo la kuficha na kwamba yanayosemwa na baadhi ya wanasiasa ni uzushi, chuki, na uongo.
Rais Dkt. Mwinyi amewataka wananchi kuwadharau wanasiasa wanaoleta sera za ubaguzi badala ya kueleza sera za maendeleo.

Kwa upande mwingine, Wabunge na Wawakilishi wa Mkoa wa Kusini Pemba wamemchangia shilingi milioni moja Rais Dk. Mwinyi kwa ajili ya fomu ya kugombea nafasi ya Urais wa Zanzibar mwaka 2025.