DAR-Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi ya NBC Tanzania, Almas Kasongo amesema, baadhi ya kanuni za ligi msimu ujao wa 2024/25 ni kuwa uwanja ambao hautakuwa na viti 3,000 kwa ajili ya mashabiki hautatumika kwenye michezo ya Ligi Kuu.
Ameyasema hayo leo Agosti 6, 2024 kwenye semina ya waandishi wa habari iliyosimamiwa na bodi hiyo jijini Dar es Salaam.
Kasongo amesisitiza kuwa, viti 3,000 ndio itakuwa idadi ya chini kabisa ya viti kwenye jukwaa, huku likitakiwa eneo la kuchezea na vyumba vya kubadilishia nguo ambavyo vinakidhi viwango.
Pia ameongeza kuwa, kanuni zinazitaka klabu kuwa na wachezaji wasiopungua wawili kutoka timu za vijana watakao kuwa sehemu ya mchezo katika mechi za ligi kuu nchini.