DAWASA:Tunamshukuru Rais Dkt.Samia kwa kuchukua hatua hii

NA GODFREY NNKO

KAIMU Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA),Mhandisi Mkama Bwire ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuchukua hatua madhubuti kukabiliana na changamoto ya maji kupitia maeneo wanayohudumia.
Mhandisi Bwire ametoa shukurani hizo Agosti 7,2024 jijini Dar es Salaam katika kikao kazi na wahariri mbalimbali wa vyombo vya habari nchini chini ya uratibu wa Ofisi ya Msajili wa Hazina (TR).

"Tunaishukuru Serikali ya Mheshimiwa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuchukua hatua madhubuti ya kukabiliana na changamoto ya maji kwenye maeneo ya Dar es Salaam na Pwani.

"Ni kupitia ujenzi wa Bwawa kubwa la Kidunda litakalokuwa na uwezo wa kuhifadhi maji lita bilioni 190 ya kutumika wakati wa kiangazi ili kuepusha wananchi kukosa maji."
Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA, Mhandisi Mkama Bwire akizungumza katika kikao kazi kati ya DAWASA na wahariri, wanahabari nchini chini ya uratibu wa Ofisi ya Msajili wa Hazina Agosti 7,2024 jijini Dar es Salaam.

Mradi wa Bwawa la Kidunda ulisanifiwa wakati wa ujenzi wa mtambo wa kuzalisha maji wa Ruvu Juu miaka ya 1950, ingawa kwa kipindi cha awamu zote za Serikali kuanzia ya awamu ya kwanza mpaka Awamu ya Tano.

Aidha, mradi huu haukuweza kutekelezwa kutokana na changamoto mbalimbali ikiwemo ukosefu wa fedha.

Kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi na uharibifu wa mazingira uliokithiri katika chanzo cha Mto Ruvu, kina cha maji cha mto huo kimekuwa kikipungua hasa wakati wa kiangazi.

Hivyo kusababisha mitambo ya Ruvu Juu na Ruvu Chini kukosa kusukuma maji ya kutosha na kuleta changamoto ya huduma ya maji kwa wananchi.
Baadhi ya wahariri na waandishi wa habari wakiwa katika kikao kazi kati yao na DAWASA chini ya Ofisi ya Msajili wa Hazina Agosti 7,2024 jijini Dar es Salaam.

Lakini, kupitia Serikali ya Awamu ya Sita, inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia mradi huu wenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 329 umeanza kutekelezwa kwa kutumia fedha za ndani za Serikali na utakamilika mwaka 2026.

Maboresho

Katika hatua nyingine, Mhandisi Bwire amesema, DAWASA imefanya maboresho mbalimbali yenye lengo la kuleta ufanisi wa kuhudumia wateja, ambapo wamepata mafanikio makubwa katika uzalishaji na uanzishaji wa miradi mipya.

Amesema,kwa sasa uzalishaji wa maji kwa DAWASA umeongezeka kutoka lita milioni 520 kwa siku hadi lita milioni 534.6 kwa siku, sawa na ongezeko la lita milioni 14.6 kwa siku.

Mhandisi Bwire amesema, mbali na kuongezeka kwa uzalishaji maji, pia uwezo wao wa kuhifadhi maji umeongezeka kutoka lita milioni 154 hadi lita milioni 184 sawa na ongezeko la lita milioni 30.
Baadhi ya wahariri na waandishi wa habari wakiwa katika kikao kazi kati yao na DAWASA chini ya Ofisi ya Msajili wa Hazina Agosti 7,2024 jijini Dar es Salaam

“Uwezo wa uzalishaji maji umeongezeka kutoka lita milioni 520 kwa siku mpaka lita milioni 534.6 kwa siku, ambalo ni sawa na ongezeko la lita milioni 14.6 kwa siku. Hii ni pamoja na ongezeko la uwezo wa DAWASA katika kuhifadhi maji.

“Uwezo wa kuhifadhi maji umeongezeka kutoka lita milioni 153.64 hadi lita milioni 183.64 sawa na ongezeko la lita milioni 30, huku mtandao wa usafirishaji na usambazaji maji ukiwa umeongezeka kutoka kilomita 4,690.7 hadi kilomita 7,087."

Ameongeza kuwa, mtandao wa usafirishaji na usambazaji maji nao umeongezeka kutoka kilomita 4,690.7 hadi kufikia kilomita 7,087, wakati ule wa majitaka uliokuwa wa kilomita 450 kwa sasa umefikia kilomita 517.12, sawa na ongezeko la kilometa 67.12, ambapo wateja waliounganishwa majisafi wameongezeka kutoka 343,019 hadi 438,177.


Miradi

Mhandisi Bwire amesema,miradi mipya inayoendelea kutekelezwa ni pamoja na mradi wa maji Dar es Salaam ya Kusini, uliosainiwa Oktoba 31, 2023, ambao ni ujenzi wa tenki la ujazo wa lita milioni tisa, wenye thamani ya shilingi bilioni 34.5.
Baadhi ya watendaji wa DAWASA, wahariri na waandishi wa habari wakiwa katika kikao kazi kati yao na DAWASA chini ya Ofisi ya Msajili wa Hazina Agosti 7,2024 jijini Dar es Salaam.
"Kwa sasa tunaendelea na utekelezaji wa mradi mkubwa wa kusambaza maji maeneo ya Dar es Salaam ya Kusini ambao unalenga kunufaisha majimbo matano ya uchaguzi ikiwemo Ukonga, Ubungo, Kibamba, Segerea na Ilala.

"Mradi unajenga tenki kubwa la lita milioni 6 na unagharimu bilioni 34.5, mradi huu unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwaka huu."

Vile vile, Mhandisi Bwire amesema kuwa kuna jumla ya matanki 138 yenye uwezo wa kuhifadhi maji lita 183,649,000 na kuweza kutoa huduma kwa saa zisizopungua sita.

Amesema kuwa, kutokana na uhitaji bado wanahitaji nguvu kutoka sekta binafsi ya kuongeza vyanzo vya maji, huku akieleza kuwa hivi karibuni wanatarajia kupata vyanzo vingine kutoka Mto Rufiji, pamoja na bwawa hilo.
Baadhi ya watendaji wa DAWASA wakiwa katika kikao kazi kati yao na DAWASA chini ya Ofisi ya Msajili wa Hazina Agosti 7,2024 jijini Dar es Salaam.

“Kila palipo na mafanikio, changamoto hazikosekani, iko hivyo pia kwa DAWASA inapambana na changamoto mbalimbali zikiwemo za mabadiliko ya tabia nchi,uvamizi na uharibifu wa vyanzo vya maji.

“Changamoto zingine zinazoikabili DAWASA ni pamoja na ujenzi wa makazi usiozingatia taratibu za mipango miji, ushirikiano na wadau kutatua changamoto na uvamizi katika maeneo ya hifadhi ya miundombinu ya maji.

"Kuhusu suala la upotevu wa maji kwa wateja, mamlaka imeanza na inaendelea na zoezi la kufunga mita kubwa kwa lengo la kupima kiasi cha maji kinachozalishwa na kinachotumika."
Baadhi ya wahariri na waandishi wa habari wakiwa katika kikao kazi kati yao na DAWASA chini ya Ofisi ya Msajili wa Hazina Agosti 7,2024 jijini Dar es Salaam.

Amesma, ni ili kubaini kiasi cha maji yanayopotea mitaani na kudhibiti kwa lengo la kuboresha huduma. "Zoezi limeanza Kinondoni na linaendelea eneo la Kawe na Tabata."

TR

Akiongoza kikao kazi hicho, Afisa Habari Mwandamizi kutoka Ofisi ya Msajili wa Hazina, Sabato Kosuri amesema, kikao hicho ni mwendelezo wa vikao kazi kati ya wahariri yakiwemo mashirika na taasisi zilizopo chini ya ofisi hiyo.
Afisa Uhusiano Mwandamizi kutoka Ofisi ya Msajili wa Hazina Sabato Kosuri akizungumza katika kikao kazi hicho Agosti 7,2024 jijini Dar es Salaam.

Sabato amesema, vikao hivyo licha ya kuwapa uwanda mpana viongozi wa mashirika na taasisi husika kuelezea walipotoka, walipo na wanapoelekea pia wanaelezea mafanikio waliyoyapata na mikakati waliyonayo.

Aidha,amewakumbusha wahariri na waandishi wa habari umuhimu wa vikao kazi hivyo, huku akiwataka kuzingatia yale yote yanayowasilishwa ili kupelema elimu sahihi kwa umma.

TEF

Naye,Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tazania (TEF), Deodatus Balile licha ya kuipongeza DAWASA kwa jitihada kubwa wanazoendelea nazo za kuzalisha na kusambaza maji, pia amesehauri.

“Upotevu wa maji ni mkubwa, utakuta mitaani kumetapakaa maji na kuzalisha madimbwi makubwa.

"Lakini hakuna hatua za makusudi zinachokuliwa kwa haraka kuzuia uharibifu huo. Upotevu wa maji hauepukiki katika usambazaji wa maji, lakini unaoshuhudiwa ni mkubwa sana.
Baadhi ya wahariri na waandishi wa habari wakiwa katika kikao kazi kati yao na DAWASA chini ya Ofisi ya Msajili wa Hazina Agosti 7,2024 jijini Dar es Salaam.

“Tunatamani kuona DAWASA muende mbali zaidi mufunge mita za maji kila mtaa, kila kata, hii itasaidia kuona haya maji yanapotelea wapi.

"Na katika hili la smart meter, nashauri taasisi iangalie mita zinazotengenezwa na wazawa, hizi za kigeni hazina ubora."

Madeni

Wakati huo huo, Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA,Mhandisi Mkama Bwire amesema, mamlaka hiyo inadai zaidi ya shilingi bilioni 40 kutoka kwa wateja wake mbalimbali kuanzia taasisi hadi mteja mmoja mmoja.
Baadhi ya wahariri na waandishi wa habari wakiwa katika kikao kazi kati yao na DAWASA chini ya Ofisi ya Msajili wa Hazina Agosti 7,2024 jijini Dar es Salaam.

"Ni kweli bado tuna madeni ambayo yapo, tunaangalia inakwenda takribani bilioni 40 kwa ujumla wake,lakini katika hiyo bilioni 40 ninaweza kusema imegawanyika katika makundi matatu.

"Kwa taasisi mbalimbali inaenda karibu bilioni 22, halafu kundi la pili ni madeni ambayo yanatokana na wateja ambao wameshaondolewa huduma karibu bilioni 15.

"Halafu la tatu ni wateja wa majumbani ambao wanadaiwa bili ya maji karibu bilioni 10, lakini kulingana na Sera yetu ya ufuatiliaji wa madeni, hayo bado ni himilivu yaani bado yapo ndani ya muda ambao tunasema kwamba yanalipika kwa wateja ambao bado wanapata huduma.
Baadhi ya wahariri na waandishi wa habari wakiwa katika kikao kazi kati yao na DAWASA chini ya Ofisi ya Msajili wa Hazina Agosti 7,2024 jijini Dar es Salaam.

"Kwa sababu kuna muda ukifika utasema hili deni siyo himilivu. Sasa ukichukua kwa wastani katika biashara ya maji, deni letu hili la takribani bilioni 40 kwa DAWASA linaweza lisiwe la kutisha sana kwa sababu huwa tunalipima katika kipimo cha wastani.

"Hili deni ni sawasawa na bili karibu za miezi mitatu, yaani ndiyo unaliona linakuwa hapo, sasa huwa linaanza kuwa na dalili ambazo siyo nzuri pale deni liliko nje linaanza kuwa ni la bili ya miezi sita kwenda mbele."

Hata hivyo,Mhandisi Mkama Bwire amesema, mamlaka hiyo imejiwekea mikakati thabiti ya kufuatilia madeni yote ili kuhakikisha yanalipwa yaweze kusaidia kutekeleza miradi mingine ya maji.

"Kila kundi lina mikakati yake ya kulifuatilia, kwenye taasisi ninafikiri hii approach ninafikiri ya madeni ya nyuma ya hawa wateja, tutakapoenda kwenye prepaid meters sasa hivi yatatoka na approach tutakayoitumia tukishakufungia mita kama ulikuwa na deni tutakubaliana asilimia ya maji unayonunua ya muda huo asilimia fulani itakuwa inakatwa kwenye deni lako la nyuma.
Baadhi ya wahariri na waandishi wa habari wakiwa katika kikao kazi kati yao na DAWASA chini ya Ofisi ya Msajili wa Hazina Agosti 7,2024 jijini Dar es Salaam.

"Pindi ukiendelea kupata huduma,kwa mfano tunaweza kusema kwa mwezi ukanunua maji ya shilingi laki moja,lakini ulikuwa na deni.


"Kwa hiyo hautapata maji ya shilingi laki moja utapata maji kama tumekubaliana asilimia 20, utapata maji ya shilingi 80,000 na elfu ishirini itakata deni la nyuma.

"Kwa hiyo baada ya muda automatically yale madeni yatakuwa yameisha na utaendelea kutumia huduma kwenye bili ya kawaida."

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news