DCEA yafikisha elimu kwa viongozi mbalimbali Arusha

NA GODFREY NNKO

MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) Kanda ya Kaskazini imetoa elimu kwa viongozi mbalimbali wa Serikali kutoka halmashauri saba za Mkoa wa Arusha.
Ni kupitia kikao kazi cha usimamizi wa mitihani ya Taifa kilichofanyika katika ukumbi wa ofisi ya mkuu wa mkoa huo Agosti 16,2024.

Mkoa huo unaundwa na Halmashauri ya Jiji la Arusha,Halmashauri ya Arusha,Halmashauri ya Meru,Halmashauri ya Monduli,Halmashauri ya Karatu, Halmashauri ya Longido na Ngorongoro.

Akizungumza katika kikao hicho, Afisa Ustawi wa Jamii Mwandamizi wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) Kanda ya Kaskazini, Bi. Sara Ndaba amesema,kikao kazi hicho ni muhimu katika kufikisha elimu juu ya dawa za kulevya.
"Tumeona hadhira hii ni muhimu sana kwetu kwa sababu kile ambacho utakifahamu kuhusu Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, basi kitakufanya uwiwe kutualika kwenye maeneo ambayo mnatoa huduma ili tuweze kutoa elimu hii."

Bi.Ndaba amesema, mikakati ya Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) ni pamoja na kuzuia usambazaji na uhitaji wa dawa za kulevya (supply reduction) nchini."Lakini mkakati wa pili ni demand reduction ambayo ndiyo hiyo sasa tunatoa elimu kuzuia uhitaji wa hizo dawa za kulevya.

"Kwa hiyo, kwa kundi hili ambalo tumekutana nalo leo, tunaamini kabisa mnaishi na watoto, mnafanya kazi na watoto ambao tunawategemea kuwa watu bora au viongozi bora wa baadae, hivyo ujumbe huu ni sehemu sahihi kabisa."

Vile vile, kupitia kikao kazi hicho ambacho kiliwaleta pamoja washiriki zaidi ya 50 wakiwemo maafisa elimu na taaluma wa mkoa na halmashauri wa shule za msingi na sekondari,maafisa sheria wa halmashauri,
Maafisa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), maafisa usalama wa taifa wilaya, makamanda wa polisi wa wilaya wote kwa pamoja walikumbushwa wajibu wao wa kupambana na dawa za kulevya.

Sambamba na kushirikiana na Mamlaka ya Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya ikiwemo kutoa taarifa kuhusu wahalifu wa dawa za kulevya.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news