DCS yawapiga msasa wakurugenzi wa mikoa na maafisa uhusiano na masoko wa OUT

DAR-Kurugenzi ya Huduma za Ushauri wa Kitaalamu ya Chuo Kikuu Huria Cha Tanzania (DCS) kwa kushirikiana na OUT Consultancy Bureau (OCB) imeendesha mafunzo ya kuwajengea uwezo wa kutafuta na kufanya kazi za kutoa huduma za ushauri wa kitaalamu na kuendesha kozi fupi fupi wakurugenzi wa vituo vya mikoa pamoja na maafisa uhusiano na masoko wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT).
Sehemu ya picha zilizopigwa kwenye mafunzo hayo yaliyofanyika kwa njia ya Zoom.

Mafunzo hayo yamelenga kuwaongezea mbinu za kutambua fursa zilizopo katika maeneo yanayowazunguka hasa huko vituo vya mikoa vilipo ikiwamo kuzitambua changamoto na fursa mbalimbali katika jamii wanazoishi na kujua njia bora ya kuzitatua ili kuisaidia jamii husika.
Akifungua mafunzo hayo, Kaimu Naibu Makamu Mkuu wa Chuo (Teknolojia za Kujifunzia na Huduma za Mikoa), Profesa Leonard Fweja, amewataka washiriki kutumia fursa hiyo adhimu kuongeza maarifa ya kuisadia jamii inayowazunguka kutatua changamoto mbalimbali.

Amekumbusha pia kufanya kazi za kutoa huduma ya ushauri wa kitaalamu kwa jamii ni kutekeleza moja ya jukumu mama la Chuo Hikuu Huria cha Tanzania.

Pia, ni sehemu ya kukiongezea chuo mapato na mtumishi husika kunufaika moja kwa moja na sehemu ya mapato hayo, kupata uzoefu katika tasnia yake na kuchangia katika upandaji wa ngazi za kitaaluma kwa upande wa walimu.

Aidha, Prof. Fweja ameipongeza Kurugenzi ya Huduma za Ushauri wa Kitaalamu inayoshirikiana na OCB kwa fursa ya mafunzo hayo na kutoa rai ya kufanya hivyo mara kwa mara ili kuongeza ufanisi kwa watumishi wa OUT na huduma watoazo kwa jamii.

Mafunzo hayo yaliratibiwa na Mkurugenzi wa DCS, Dkt. Edephonce Nfuka akishirikiana na Watumishi wote wa Kurugenzi hiyo pamoja na OCB.

Watoa mada kwenye Mafunzo hayo yaliyojikita kwenye elimu ya jumla kuhusu namna zitolewavyo na chuo huduma hizi za ushauri wa kitaalamu na kozi fupi pamoja na uzoefu na mbinu za kutumia hasa huko vituo vya mikoa vilipo walikuwa ni Mkurugenzi wa DCS, Dkt. Nfuka na Dkt. Nasra Kara (Mratibu wa Huduma za Ushauri wa Kitaalamu na Jamii) akishirikiana na Bw. Mwanuzi Babyegeya katika eneo hilo.

Pia,Dkt. Karol Mrema (Mratibu wa mafunzo mafupi ya ndani na ya wateja wa nje) akishirikiana na Bw. Revocatus Biro katika eneo hilo walisistiza vitu vya muhimu katika kutayarisha, kusajili, kuendesha, kutangaza na kutathmini kozi fupi.
Watoa mada wengine walikuwa wale wa kutoka nje ya DCS waliozama kwenye uzoefu na mikakati ya kuwezesha kupatikana na kuziendesha huduma hizi huko vilipo vituo vyetu vya mikoa yaani Dkt. Emmanuel Mallya (Mkuu wa OCB), Bw. Dennis Semiono (Mkurugenzi, Kituo Cha Mkoa wa Kilimanjaro), Dkt. Nangware Msofe (Mkurugenzi, Kituo Cha Mkoa wa Arusha) na Bi. Mwajuma Mmasi, Afisa Uhusiano na Masoko (Kituo Cha Mkoa wa Pwani).

Mafunzo hayo yalikuwa shirikishi ambapo washiriki walipewa fursa ya kutoa uzoefu wao, nafasi ya kuchangia kwa kutoa maoni na kuuliza maswali kwa uelewa zaidi.

Akitoa salamu za kufunga mafunzo haya yaliyofanyika Agosti 29,2024 na kuhudhuriwa na washiriki 57 kutoka vituo mbalimbali vya OUT, Dkt. Adam Namamba, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Masoko wa OUT, amewataka watumishi waliopata fursa ya mafunzo hayo na kukutana pamoja kwa jinsi hii kuonesha mabadiliko kwa vitendo kwa kuongeza shughuli hizi za huduma za ushauri wa kitaalamu na kozi fupi.

Alihitimisha kwa kutanabaisha kuwa yeye pamoja na timu ya Maafisa Uhusiano na Masoko wa OUT ambao wapo chini yake wapo tayari kushirikiana na DCS pamoja na mshirika wake OCB muda wote ili kuongeza juhudi za kukiletea mafanikio chuo hiki na mtumishi mmoja mmoja.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news