Diaspora wahimizwa kutoa maoni Dira ya Maendeleo 2050

NEW YORK-Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenye Umoja wa Mataifa, Mhe. Hussein A. Kattanga amewasihi Watanzania wanaoishi nje ya nchi (diaspora) kutoa maoni kwenye Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050 ambapo Serikali imetoa kiunganishi (link) maalum kwa Diaspora kutoa maoni yao.
Balozi Kattanga alitoa rai hiyo kwenye tafrija ya nyama choma maarufu kama Summer Barbaque iliyondaliwa na Jumuiya ya Watanzania waishio jijini New York, New Jersey, Pennsylvania na Connecticut iliyofanyika Agosti 10, 2024.
Balozi Kattanga ambaye alikuwa Mgeni Rasmi kwenye tafrija hiyo alisema kuwa maoni yao ni muhimu ili kuhakikisha hakuna mtu au kundi la watanzania linaloachwa nyuma kwenye mchakato wa kuandaa Dira hiyo.

Lengo la tafrija hiyo lilikuwa ni kuwaleta pamoja watanzania waishio maeneo hayo ili kufahamiana, kushirikishana fursa mbalimbali za kazi na biashara na kujadiliana namna wanavyoweza kuchangamkia fursa mbalimbali zilizopo nyumbani nchini Tanzania.

Balozi Kattanga aliwasisitiza wanajumuiya hao kudumisha upendo baina yao, kushirikishana fursa mbalimbali zinazopatikana katika maeneo wanayoishi nchini Marekani, kuchangamkia fursa mbalimbali zilizopo nchini Tanzania kama vile uwekezaji, ununuzi wa nyumba kupitia Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) na mashirika mengine yanayojihusisha na biashara hiyo na ununuzi wa hisa kwa ajili ya kujiwekea akiba zao za baadaye na kukumbuka kusaidia familia zao zilizopo nchini Tanzania.
Vilevile, aliwasisitiza kufuata sheria za nchi wanayoishi ili kuepuka kupata matatizo mbalimbali yanayotokana na ukiukwaji wa sheria za nchi husika.

Kwa upande wake Kaimu Mwenyekiti ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo Bw. Gaston Mkapa, alitumia fursa hiyo kuwahamasisha Wanajumuiya kuendelea kudumisha umoja, upendo na mshikamano. 

Vilevile, alisisitiza kusajili taarifa za wanajumuiya hao kwenye tovuti ya jumuiya ili kuiwezesha Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa na taarifa zao kuhusu taaluma na kazi zao na kuwezesha balozi za Tanzania nje kuwahudumia ipasavyo pale inapohitajika kufanya hivyo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news