Diwani ahukumiwa kifungo cha miaka 20 jela kwa ubadhirifu

MWANZA-Mahakama ya Wilaya ya Ukerewe imemhukumu Diwani wa Kata ya Illangala, Petro Misana Majula adhabu ya kutumikia kifungo cha miaka 20 jela.
Ni baada ya kukutwa na hatia katika makosa ya Ufujaji, Ubadhirifu pamoja na Matumizi Mabaya ya Mamlaka, kinyume na vifungu vya 28 (1) pamoja na 31 vyote vya Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa [CAP 329 R.E 2022].

Vifungu ambavyo vinasomeka pamoja na Aya ya 21, Jedwali la kwanza, pamoja na vifungu vya 57(1) na 60(2) na (3) vya Sheria ya Uhujumu Uchumi Sura ya 200 kama ilivyofanyiwa Marejeo Mwaka 2022.

Hukumu dhidi ya Bw. Petro Majula Misana imetolewa Agosti 5, 2024 kutokana na Shauri la Uhujumu Uchumi Na. 02/2023 lililokuwa katika Mahakama ya Wilaya ya Ukerewe mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Lucas Nyahenga.

Shauri hili liliendeshwa na Mwendesha Mashtaka kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Mwanza Bw. Moses Malewo.

Awali ilielezwa kuwa Mshtakiwa alifikishwa Mahakamani hapo kwa mashtaka tajwa hapo juu kwa kushindwa kuwasilisha kiasi cha shilingi 5,198,546.80 katika akaunti ya Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe, fedha ambazo alizikusanya kutoka kwenye vyanzo mbalimbali vya mapato vya halmashauri hiyo akiwa wakala wa kukusanya mapato.

Bw. Petro Misana Majula alifanya hivyo huku akijua ni kinyume na Memoranda ya Fedha za Halmashauri za Mwaka 2009 lakini pia ni Kinyume na Sheria ya Fedha za Halmashauri Sura ya 290 kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2019.

Sheria hizi zote zinamtaka kila anayekusanya mapato ya halmashauri kuyawasilisha kwenye akaunti za halmashauri kila siku anapokusanya ama kesho yake endapo kuna changamoto.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news