Dkt.Kiruswa ataja sababu za maboresho Kanuni za CSR

DODOMA-Naibu Waziri wa Madini, Mhe. Dkt. Steven Kiruswa amesisitiza kuwa,maboresho ya Kanuni na Wajibu wa Wamiliki wa Leseni za Madini kwa Jamii (CSR) za mwaka 2023 yamelenga kuhakikisha kunakuwa na ushirikishwaji wa pamoja.
Ni kati ya jamii na kampuni za Madini katika utekelezaji wa miradi ya jamii, jambo ambalo ni muhimu kwa maendeleo endelevu ya jamii zinazozunguka migodi.

Ameyasema hayo Agosti 15, 2024 wakati akifungua Kikao cha maboresho ya Kanuni hizo, kilichofanyika katika Ukumbi wa St. Gasper jijini Dodoma.
Kikao hicho kimewakutanisha wadau mbalimbali wakiwemo Wamiliki wa Leseni (Makampuni ya Uchimbaji), wataalam kutoka Halmshauri mbalimbali nchini ambako shughuli za madini zinafanyika kwa wingi.Washiriki wengine ni pamoja na Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Wabunge, Wenyeviti na Wakurugenzi wa Halmashauri ambapo shughuli za uchimbaji wa madini zinafanyika, Taasisi za Umma, Vyama vya Wachimbaji pamoja na Asasi za kiraia.
Dkt. Kiruswa amesema kuwa, tangu mwaka 2017, baada ya Sheria ya Madini ya mwaka 2010 kufanyiwa marekebisho na kuongezwa kifungu cha 105 kinachohusu wajibu wa Kampuni kwa jamii, Sekta ya Madini imeona mafanikio makubwa na kwamba licha ya mafanikio hayo, utekelezaji wa Kanuni za CSR umekuwa na changamoto kadhaa ambazo zinahitaji kushughulikiwa kupitia maboresho.

"Ndugu Washiriki, changamoto hizo ni pamoja na Mipango ya miradi ya CSR kutoandaliwa kwa wakati na ile miradi iliyoandaliwa kutotekelezwa kwa wakati; Kukosekana kwa miongozo ya utekelezaji wa mipango ya CSR ambayo kwa mujibu wa Sheria inapaswa kuandaliwa na Mamlaka ya Serikali za Mitaa kwa kuwashirikisha Wamiliki wa Leseni za Madini.”
Ametaja changamoto zingine kuwa ni kupishana kwa mitazamo kati ya Halmashauri na Wamiliki wa Leseni za Madini kuhusiana na aina ya miradi na namna ya kuitekeleza pamoja na uelewa mdogo wa masuala za CSR kwa jamii pamoja na migogoro baina ya Wamiliki wa Leseni za Madini na Mamlaka za Serikali za Mitaa hali inayopelekea baadhi ya miradi ya kijamii kutokukidhi mahitaji na matarajio ya jamii zinazozunguka migodi.

Katika hatua nyingine, Dkt. Kiruswa amesisitiza kuwa Wizara ya Madini inaendelea kuhamasisha kampuni za madini kuongeza michango yao kwa jamii kupitia miradi ya CSR.
Ameeleza kuwa, kwa kipindi cha Mwaka 2018 hadi 2023, Kampuni za Madini zimechangia zaidi ya shilingi bilioni 96.6 za Kitanzania kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo ya jamii na kwamba mchango huo bado unaweza kuongezeka ikiwa changamoto zilizopo zitashughulikiwa ipasavyo na ushirikiano kati ya kampuni na jamii utaimarishwa.
Kwa upande wake, Kamishna wa Madini, Dkt. AbdulRahman Mwanga amesema kuwa Kikao hicho ni kinatambuliwa na Sheria ya Madini.

“Tunapofanya uvunaji wa Madini, tunaona tuwe na utaratibu wa kurejesha kwa Jamii ili kujenga mahusiano mazuri na kulinda biashara na shughuli za Madini zifanyike vizuri, Wizara inaona ni vizuri kupokea maoni ili kuboresha Kanuni hizi.”
Ameongeza kwamba, maoni yatakayopatikana katika kikao hicho yatasaidia kupunguza changamoto zilizopo na kuhakikisha kuwa sekta ya madini inaendelea kuleta manufaa kwa Watanzania na taifa kwa ujumla.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news