ARUSHA-Naibu Katibu Mkuu (ELIMU) Ofisi ya Rais TAMISEMI, Dkt. Charles Msonde amewataka Watendaji wa Mikoa, Halmashauri na ngazi ya msingi kuwa waadilifu, kujiamini na kufuatilia miradi ya maendeleo ili kuleta ufanisi na kulinda thamani ya fedha za Serikali.
Dkt. Msonde ametoa kauli hiyo Julai 31, 2024 katika Chuo cha Ualimu Patandi jijini Arusha wakati akifunga mafunzo ya siku tatu kwa Maafisa Elimu mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Manyara na Tanga, Maafisa TEHAMA na Waratibu wa Mradi ngazi ya Mkoa,
Maafisa Elimu Sekondari, Maafisa Manunuzi na Ugavi ngazi ya Halmashauri, Waratibu wa mradi ngazi ya Halmashauri na Wakuu wa Shule kuhusu utekelezaji wa miradi ya shule za sekondari (SEQUIP).
“Niwatake wasimamizi na wataalamu wote wa elimu na Idara mwambata katika usimamizi wa Miradi mkaimarishe usimamizi na kuongeza ubunifu katika utatuzi wa changamoto zinazoathiri shughuli za ujenzi wa miundombinu ya shule.
"Aidha, mkasimamie vema utekelezaji wa maboresho yanayofanyika mara kwa mara katika shughuli za ujenzi kwenye maeneo yenu,” alisema Dkt. Msonde.
Dkt. Msonde amewataka watendaji hao kuhakikisha ujenzi wa miundombinu inakamilika kabla au ifikapo Novemba 1, 2024 ili shule zinazojengwa zisajiliwe na kuwekwa katika mpango wa kuwapokea wanafunzi kwa ajili ya kuanza masomo mwaka 2025.
Sambamba na kuzingatia thamani ya fedha na Wakuu wa Shule na Waratibu Elimu Kata watakaoshindwa kusimamia wataondoshwa kwenye nafasi zao.
Akitoa maelezo ya awali, Mratibu Mradi wa SEQUIP kutoka Idara ya Usimamizi wa Elimu Ofisi ya Rais TAMISEMI Bw. Robert Msigwa amesema mafunzo hayo yamehusisha jumla ya washiriki 240 wakiwemo Maafisa Elimu sekondari 32, Maafisa Ugavi wa Halmashauri 35 na Wakuu wa shule 124 kutoka shule za sekondari zilizopokea fedha za awamu ya tatu kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu shuleni.
Aidha, Bw. Msigwa amesema, Ofisi ya Rais TAMISEMI ilibaini uwepo wa changamoto ya usimamizi na uzingatiaji wa miongozo mbalimbali ya usimamizi wa ujenzi na suluhisho likawa kuwajengea uwezo maafisa hao ili kuimarisha usimamizi wa ujenzi wa miundombinu ya Serikali.
Naye Mkuu wa Shule Kwaraa Sekondari kutoka Babati Mji Deogratius Ami amesema mafunzo hayo yatawasaidia kutekeleza miradi ya ujenzi kwa wakati na ufanisi mkubwa na kuzingatia maelekezo ya Serikali ikiwa ni pamoja na kushirikiana na Maafisa wengine kwa mujibu wa mifumo ya manunuzi na dhana ya ufuatiliaji miradi (Kobo tool).
Mafunzo ya kuwajengea uwezo Maafisa hao yamefanyika katika vituo sita ambapo awamu ya kwanza yalifanyika katika vituo vya Chuo cha Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima Morogoro, Chuo cha Ualimu Mtwara na chuo cha Ualimu Butimba na awamu ya pili tikifanyika Chuo cha Ualimu Patandi, Tabora na Mbeya.