ZANZIBAR-Sheha wa Tumbatu Uvivini ndugu Ngwali Sheha Haji, amesema miongoni mwa changamoto zinazopelekea kutokuwepo ushiriki sawa wa kijinsia katika michezo ni pamoja na kukosekana kwa miundombinu rafiki na skuli kutokua na muda maalum wa michezo kwa wanafunzi.
Sheha Ngwali amesisitiza kuwa mila na desturi sio kikwazo kwani historia inaonesha kuwa kuna wanawake mbalimbali kutoka kisiwani hapo ambao wamewahi kushiriki michezo na kuwa vinara katika kisiwa hicho.
Sheha wa Tumbatu Uvivini ndugu Ngwali Sheha Haji akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani).
“Hapo zamani miaka ya 1973 wakati mimi ni mwanafunzi kulikuwepo wanawake wanaoshiriki michezo na kuchukua medali nyingi lakini ushiriki umepungua kutokana na changamoto za ukosefu wa mazingira rafiki ya kushiriki michezo kwa watoto wa kike”, alisema Sheha Ngwali.
Nae Mwalimu mkuu msaidizi skuli ya Tumbatu Msingi “A” ameeleza kuwa skuli hiyo ina mikakati ya kuwahamasisha watoto wa kike kushiriki michezo hususan baada ya kukamilika viwanja rafiki vya michezo kupitia mradi wa michezo kwa maendeleo
Kwa upande wa wanafunzi wa kike wanaoshiriki michezo hasa mpira wa mikono (netball) katika skuli hiyo wamesema kushiriki kwao katika michezo kumewasaidia kuimarisha afya zao, kutembea sehemu mbalimbali pamoja na kupata zawadi.
Pia wameiomba serikali na wadau mbali mbali kuwaunga mkono kwa kuwasaidia vifaa mbalimbali vya michezo ikiwemo mipira, jezi na vyenginevyo ili iwe rahisi kwa wao kushiriki katika michezo.
Katika muendelezo wa utekelezaji wa mradi wa michezo kwa maendeleo, Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania Zanzibar (TAMWA ZNZ) kimefanya ziara maalum pamoja na waandishi wa habari kutembelea kisiwa cha Tumbatu kuangalia hali ya michezo katika kisiwa hicho.
Akizungumza katika ziara hiyo Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano TAMWA ZNZ, Sophia Ngalapi amesema kazi kubwa ya TAMWA ZNZ ni kutetea haki za wanawake na watoto pamoja na kukuza usawa wa kijinsia katika kila sekta ndani ya jamii.
Ameeleza kuwa lengo la ziara hiyo ni kuangalia hali ya kimichezo ndani ya kisiwa cha Tumbatu ikiwemo ushirikishwaji wa jinsia zote katika michezo, miundo mbinu pamoja na kupata maoni kutoka kwa wakaazi wa kisiwa hicho juu ya ushiriki wa watotot wa kike katika michezo bila kuharibu mila, desturi na silka za wazanzibari.