FCS na TCRA CCC zaingia makubaliano

DAR-Taasisi ya The Foundation for Civil Society (FCS) wametia saini makubaliano ya miaka mitatu na Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Mawasiliano la Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA CCC) katika kuhakikisha juhudi za kulinda haki za watumiaji wa huduma katika Sekta ya Mawasiliano nchini zinaimarika.
Akizungumza katika hafla ya kutiliana saini makubaliano hayo, yaliyofanyika Agosti 6,2024 jjini Dar es salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa FCS, Justice Rutenge amesema kuwa, ushirikiano huo unatambua umuhimu wa kuwalinda watumiaji dhidi ya mbinu za kibiashara zisizo za haki katika soko.
Amesema, jitihada za kulinda haki za Watumiaji (consumer protection) kunachangia Maendeleo ya masoko na ukuaji wa Biashara.

“Biashara zinazoheshimu sera za kulinda Watumiaji na kuwapa wateja wao kipaumbele hujijengea hadhi na kuziweka katika nafasi nzuri kiushindani.

“Kuna umuhimu wa asasi za kiraia kushiriki katika kuimarisha mifumo ya kulinda na kutetea haki za Watumiaji wa huduma na bidhaa za Mawasiliano,” amesema.
Amefafanua kuwa,katika soko la sasa lenye mabadiliko ya haraka, uadilifu katika biashara unategemea kwa kiasi kikubwa kulinda haki za watumiaji dhidi ya mbinu zisizo za haki na udanganyifu katika biashara.

“Wafanyabiashara wananafasi muhimu katika kuhakikisha uwazi na usahihi katika shughuli zao,kutoa taarifa sahihi na kwa wakati na kuepuka upotoshaji kuhusu bidhaa na huduma zao,” amesema.

Amesema,kupitia mradi huo watajenga uwezo wa asasi za kiraia kuboresha uwiano katika Sera na hatua zinazochukuliwa katika ngazi ya chini, hasa pale ambapo wadau na Watumiaji wa bidhaa wana uelewa mdogo kuhusu haki na majukumu yao ili kukuza uelewa wa watumiaji wa huduma na bidhaa.

“Watumiaji wanahaki ya kupata suluhu ya haki kwa madai ya msingi, elimu na uwezo kuhusu bidhaa, huduma na haki zao na uhakika wa ubora wa bidhaa na huduma,” amesema.
Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa TCRA CCC,Mary Msuya amesema baraza limeanzishwa kwa lengo la kuwakilisha maslahi ya watumiaji wa huduma za Mawasiliano za TEHAMA, huduma za Utangazaji, huduma za posta, na vifurushi na vipeto.

Amesema, baraza linatekeleza majukumu yake ya kuwakilisha watumiaji wa huduma na bidhaa za Mawasiliano kwa kushauriana na wadau ambao ni Serikali, TCRA, watoa huduma na watumiaji wenyewe.

“Huduma za mahusiano nchini zinaongezeka kutokana na ukuaji wa kasi wa teknolojia ambapo kwa mujibu wa TCRA kufikia June 2024 kuna Kadi za simu Milioni 76.6, watumiaji wa interneti milioni 39.3, akaunti za pesa mtandao milioni 55.7.
Idadi hii itaendelea kuongezeka na huduma mpya zitaongezeka kutokana na kukua kwa teknolojia ya kidigitali.

“Ukuaji huu wa teknolojia ni muhimu hasa wakati nchi yetu imejikita kwenye uchumi wa kidigitali, mawasiliano yanawezesha kufikisha taarifa kwa wakati, uendeshaji wa shughuli mbalimbali za kijamii ikiwemo biashara, uzalishaji, elimu, afya na upatikanaji wa huduma jumuishi za kifedha,” amesema.

Hatua hiyo ya FCS na TCRA-CCC unalenga kuhakikisha kunakuwepo haki na uwajibikaji katika kutoa huduma kwa watumiaji na kuwawezesha kufanya maamuzi sahihi wanaponunua na kutumia bidhaa za huduma hiyo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news