Hayati Benjamin William Mkapa ana mchango mkubwa Sekta ya Afya nchini-Dkt.Senkoro

NA GODFREY NNKO

AFISA Mtendaji Mkuu wa Benjamin Mkapa Foundation (BMF),Dkt.Ellen Mkondya-Senkoro amesema, Rais wa Awamu ya Tatu, Hayati Benjamin William Mkapa ana mchango mkubwa katika kuimarisha Sekta ya Afya kupitia miradi ya afya ya msingi na mifumo ya utoaji huduma nchini.
Dkt.Ellen Mkondya-Senkoro ameasema hayo kupitia mahojiano na Shirika la Utangazaji la Taifa (TB1) ambapo amesema, wakati wa uongozi wake, Rais Mkapa alifanya mambo mengi huku akigusia kwa uchache mambo matatu.

Mchango wa Mkapa sekta ya afya

"Ninafikiri mchango wake unatambulika toka akiwa katika Awamu ya Tatu kama Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuanzia mwaka 1995 mpaka mwaka 2005.

"Na mtakumbuka wakati wa uongozi wake ni vingi alifanya vya sekta ya afya, lakini nitazungumzia vitatu. Kwanza ni lile ambalo wakati wa awamu yake changamoto ya UKIMWI ilijitokeza."

Ameeleza kuwa,Rais Mkapa kwa kulitambua hilo aliona ni muhimu kuweka kipaumbele katika kupambana na ugonjwa wa UKIMWI.

"Na utakumbuka kwamba suala la UKIMWI lilikuwa ni lazima lihuhishwe kwenye sekta zote. Na lisiwe tu katika Wizara ya Afya, bali kwenye makongamano, mikutano ilikuwa lazima masuala ya UKIMWI yajadiliwe.

"Lakini, kikubwa aliweza kuanzisha Kamisheni ya Kupambana na Ukimwi yaani TACAIDS mwaka 2001 kwa kupitisha sheria bungeni ya kupambana na Ukimwi.

"Pamoja na hilo, wakati huo dawa za Ukimwi zilikuwa zimeanza, lakini Tanzania tulikuwa bado hatuwezi kuzipata hata kama unaishi na Virusi Vya Ukimwi (VVU).

"Lakini, mimi ninakumbuka nikiwa kama daktari nilikuwa ninatoa huduma majumbani, nilivyohitimu kama daktari mwaka 1995.

"Nikawa ninajitolea, tunaenda tunawapa tu dawa za kupunguza makali ya maradhi mbalimbali, hatukuwa tuna ARVs.

"Kwa hiyo, Mheshimiwa Rais Mkapa akiwa Rais kwa wakati huo aliamua kutoa hela za Serikali kununua dawa za kwanza za ARVs za Tanzania ili Watanzania waweze kupata hizo dawa.Kwa hiyo hilo nafikiri ni suala la kwanza."

Pili

"Lakini,la pili tutakumbuka pia Watanzania wengi tulikuwa tunatumia cost sharing, tunatoa hela ili upate huduma ya afya.

"Kwa hiyo, wakati wa awamu yake alianzisha Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) ambayo tunaitumia sasa hivi. Na hasa ule ulikuwa umelenga kuangalia kwanza watumishi wa umma wasipate kikwazo cha kupata huduma za afya wanapotakiwa kwenda kupata huduma za afya.

"Kwa hiyo, NHIF ilianzishwa wakati wake na kama tunavyoona bado inaendelea kukuwa, lakini si hivyo tu, hata Serikali za awamu zilizokuja zimefungua wigo wa sekta binafsi kuanzishwa na kuweza kutoa huduma za bima za afya kwa Watanzania.

"Na, hata hiyo NHIF sasa imevuka si tu kwa watumishi wa Serikali imeenda pia kuwahudumia wananchi wa Tanzania wa kawaida."

Tatu

"Eneo la tatu na la mwisho, si kwamba hamna lingine, wakati Mheshimiwa Mkapa anaingia madarakani nchi yetu bado ilikuwa katika hali tete ya kiuchumi na wafadhili wengi walikuwa wamepungua katika kuleta misaada au kusaidia nchi yetu.

"Alijaribu kujenga hoja na kurudisha imani ya wafadhili na pia kuimarisha mfuko hasa wa Sekta ya Afya unaitwa Healthy Basket Fund ambapo wafadhili wanachangia kwa pamoja kwenye ule mfuko na zile fedha zinapelekwa kwenye halmashauri.

"Ili ziweze kutoa huduma za afya na huo mfuko upo mpaka leo, unaendelea na una wadau wengi wa maendeleo wanachangia kwenye huo mfuko.Kwa hiyo, hivyo ni vitu vitatu vikubwa ninaweza kusema.Endelea kutazama mahojiano hapa chini;

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news