NA LWAGA MWAMBANDE
SALIM Said Bakhresa ambaye ni mfanyabiashara maarufu, mwanzilishi na Mwenyekiti wa makampuni ya Bakhresa Group amekuwa miongoni mwa Watanzania ambao wameendelea kutoa mchango mkubwa katika huduma za kijamii na uchumi kupitia biashara zake ndani na nje ya Tanzania.
Vilevile kuchangia pato la Taifa na kuinua mapato ya familia mbalimbali ambazo zina ajira ya moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja kupitia makampuni yake.
Bakhresa Group, ambayo ni moja ya makampuni makubwa ya uzalishaji wa chakula na vinywaji hapa Tanzania na katika eneo la Afrika Mashariki.
Pia,Bakhresa amewekeza katika sekta nyingine kama usafirishaji ikiwemo katika usafirishaji wa majini, makazi na malazi, vyombo vya habari, michezo,Azam Pesa na mengineyo.
Aidha, Bakhresa kwa miongo kadhaa amechangia na anaendelea kuchangia pakubwa katika ukuaji wa uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla
Jaribu kumfikiria Said Salim Bakhresa, jinsi ambavyo anagusa maisha yetu kuanzia kwenye chakula, vinywaji, sukari, malazi, usafiri, habari, makazi, michezo na mengineyo. Bila shaka tungekuwa na Bakhresa wengi, Tanzania ingepaa zaidi kiuchumi.
Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasema, mtu kama Salim Said Bakhresa ambaye anagusa maisha ya watu wengi sana, hapa nchini na nchi za nje kutokana na bidhaa na huduma zake na kutokana na ajira, anatakiwa kuombewa kwa Mungu.
Lengo ni ili azidi kuendelea na kufanikiwa, kwani tunajua kadri anavyofanikiwa ndivyo atakavyozidi kuyagusa maisha yetu.
1. Hawa kina Bakhresa, wangekuwa wengiwengi,
Watumiao fursa, ambazo nchini nyingi,
Watu wengi kuwagusa, yale wafanyayo mengj,
Huyu tumwombee Mungu, azidi kufanikiwa.
2. Kweli anapata pesa, miradi ya kwake mingi,
Kwa huduma zake hasa, anazotoa kwa wengi,
Kwake nasi tumenasa, ajibu maswali mengi,
Huyu tumwombee Mungu, azidi kufanikiwa.
3. Chakula ni Bakhresa, bidhaa aina nyingi,
Ugali ngano twatesa, watumiaji ni wengi,
Vinywaji vingi kabisa, na machaguo ni mengi,
Huyu tumwombee Mungu, azidi kufanikiwa.
4. Sukari ni Bakhresa, watumiaji ni wengi,
Hapa kweli atugusa, wanywaji chai ni wengi,
Tena aokoa pesa, kuagiza nje nyingi,
Huyu tumwombee Mungu, azidi kufanikiwa.
5. Usafiri Bakhresa, tunaotumia wengi,
Kwenda Zenj tunatesa, maboti yalivyo mengi,
Lakini hiyo ni tisa, bado bidhaa ni nyingi,
Huyu tumwombee Mungu, azidi kufanikiwa.
6. Na Dar hatujakosa, jinsi aupiga mwingi,
Kwenda Kigamboni fursa, atusafirisha wengi,
Boti zake za kisasa, zafanya safari nyingi,
Huyu tumwombee Mungu, azidi kufanikiwa.
7. Habari ni Bakhresa, kwake tunapata vingi,
Radio ni Bakhresa, inatufikia wengi,
Kuhabarika fursa, tunapata mema mengi,
Huyu tumwombee Mungu, azidi kufanikiwa.
8. Kisimbuzi Bakhresa, chaneli twapata nyingi,
Kwake kweli tunatesa, kuyajua mambo mengi,
Tena hiyo ni fursa, wafaidi watu wengi,
Huyu tumwombee sana, azidi kufanikiwa.
9. Kwa habari Bakhresa, hizo twazipata nyingi,
Michezo ni Bakhresa, twaona mipira mingi,
Ligi zetu Bakhresa, twaona michezo mingi,
Huyu tumwombee sana, azidi kufanikiwa.
10. Hoteli ni Bakhresa, nzuri ina vyumba vingi,
Hata nyumba za kisasa, huko amejenga nyingi,
Afanya bila makosa, kweli anafanya mengi,
Huyu tumwombee sana, azidi kufanikiwa.
11. Kuwekeza Bakhresa, kodi lazima ni nyingi,
Jinsi analipa pesa, twafanyia mambo mengi,
Tena mzawa kabisa, anafanya mambo mengi,
Huyu tumwombee sana, azidi kufanikiwa.
12. Ajira ni Bakhresa, achukua watu wengi,
Maisha anayogusa, ni mamilioni mengi,
Kimaisha tunatesa, kazi zake nyinginyingi,
Huyu tumwombee sana, azidi kufanikiwa.
13. Wawe kina Bakhresa, hapa nchini ni wengi,
Tutafanikiwa hasa, tufanyapo mambo mengi,
Jinsi watu anagusa, katika sekta nyingi,
Huyu tumwombee sana, azidi kufanikiwa.
14. Twasikia Bakhresa, sadaka atoa nyingi,
Watu anaowagusa, wana shida nyinginyingi,
Kimyakimya Bakhresa, siyo kwa mabango mengi,
Huyu tumwombee sana, azidi kufanikiwa.
15. Mlaji wa Bakhresa, huduma za kwake nyingi,
Umwombee Bakhresa, azidi kufanya mengi,
Azidi wengi tugusa, nasi tufikie kingi,
Huyu tumwombee sana, azidi kufanikiwa.
16. Waje kina Bakhresa, changamoto zetu nyingi,
Wanapozipata fursa, ziwafae watu wengi,
Baraka hawatakosa, kwa maombi yetu wengi,
Huyu tumwombee sana, azidi kufanikiwa.
17. Kupitia Bakhresa, Tanzania iko kwingi,
Malawi ni Bakhresa, bidhaa zake ni nyingi,
Nako wengi awagusa, kwa shughuli za msingi,
Huyu tumwombee sana, azidi kufanikiwa.
18. Rwanda nako Bakhresa, azidi upiga mwingi,
Bidhaa huduma hasa, wanazitumia wengi,
Sifa zake zatugusa, twaeleweka na wengi,
Huyu tumwombee sana, azidi kufanikiwa.
19. Uganda ni Bakhresa, nako anafanya mengi,
Zambia Burundi hasa, anafanya mambo mengi,
Mambo yake ya kisasa, tunayoyapenda wengi,
Huyu tumwombee sana, azidi kufanikiwa.
20. Ainuke Bakhresa, nasi tufaidi mengi,
Azidi wengi tugusa, tutatue yetu mengi,
Mungu amwepushe visa, kwa hizo huduma nyingi,
Huyu tumwombee sana, azidi kufanikiwa.
(3 Yohana 1:2)
Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602