India ni mdau mkubwa wa maendeleo kwa Zanzibar-Rais Dkt.Mwinyi

ZANZIBAR-Rais ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema miongoni mwa mafanikio makubwa inayojivunia kutokana na ushirikiano wa diplomasia uliopo baina yake na Serikali ya India ni kuanzishwa kwa tawi la Chuo Kikuu cha Teknolojia cha IIT Madras, Zanzibar.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na Balozi wa India nchini Tanzania, Mhe.Bishwadip Dey, alipofika Ikulu jijini Zanzibar kwa mazungumzo na kujitambulisha leo Agosti 20,2024.(Picha na Ikulu).

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi ameyasema hayo Ikulu, Zanzibar alipozungumza na Balozi wa India nchini, Mhe. Shri Bishwadip Dey aliyefika kujitambulisha.

Amesema, Chuo Kikuu cha Teknolojia cha IIT Madras ni fursa muhimu kwa sekta ya elimu Zanzibar itakayoleta mageuzi makubwa ya mifumo na kukuza teknolojia nchini.

Dk. Mwinyi alimuhakikishia Balozi huyo ushirikiano mzuri uliopo baina ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na chuo hicho kwa kushirikiana na Serikali ya India ni jitihada zao za kuimarisha uhusiano wa Diplomasia baina yao.
Amesema, India imekua mdau mkubwa kwa maendeleo ya Zanzibar kupitia sekta mbalimbali ikiwemo miradi mikubwa ya maji safi na salama, sekta ya afya na elimu ambapo imekua ikishirikiana kwa miaka mingi.

Hivyo, ameiomba India kupitia teknolojia kubwa waliyonayo na kwa uweledi wa mitandao ya kijamii iliyobobea kuendelea kuitangaza Zanzibar Kimataifa kupitia tawi la Chuo hicho duniani pamoja na sekta za biashara na uwekezaji.

Dk. Mwinyi alisema, sekta za Afya na Elimu zimepata ushirikiano mzuri kutoka India kwa kuendelea kuwapokea Watanzania wengi kwa matibabu nchini humo sambamba na Watanzania wanaoendeleza masomo yao pamoja na ushirikiano wa biashara uliopo baina ya pande mbili za ushirikiano.

Akizungumzia sekta ya Utalii ikiwa ni sekta kiongozi ya Uchumi wa Zanzibar, Rais Dk. Mwinyi alimueleza balozi huyo kuangalia uwezekano wa kuongeza watalii wengi wa India, alimueleza balozi huyo kwamba watalii wengi wanaoingia Zanzbar ni kutoka Ulaya Mashariki na kwingineko duniani.
Naye, Balozi Shri Bishwadip alimuhakikishia Rais Dk. Mwinyi kuendeleza historia ya ushirikiano uliopo wa pande mbili hizo hasa kwenye kuboresha sekta za biashara, Uchumi, utalii na uwekezaji pia alimuahidi Rais Dk. Mwinyi kuendelea kupokea wafanyabiashara wakubwa kutoka India, wenye nia ya kuwekeza Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.

Chuo cha IIT Madsa kilianzishwa Zanzibar, mwezi Oktoba mwaka jana kwa ushiriano wa Serikali ya SMZ na Serikali ya India ambacho kinatarajiwa kuleta mageuzi makubwa kwenye sekta ya elimu, Zanzibar hasa kutoa fursa kwa wazawa ya kujifunza teknolojia.

Uhusiano wa diplomasia baina ya Tanzania na India ni wa historia ambapo India ilifungua Ubalozi wake Dar es Salaam mwezi Novemba mwaka 1962 na mwaka 1974 ikafungua ubalozi mdogo Zanzibar. Uhusiano wa pande mbili hizo umeendelea kuimarika kwa fursa nyingi za biashara na maendeleo kupatikana.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news