INEC yatoa wito kwa wananchi Manyara maboresho ya Daftari la Kudumu la Wapiga Kura

MANYARA-Wananchi mkoani Manyara wameaswa kujitokeza kujiandikisha na kuboresha taarifa zao kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwa kuwa hiyo ni haki yao kisheria.
Wito huo umetolewa na Mkurugenzi wa Habari na Elimu ya Mpiga Kura wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Bi. Giveness Aswile wakati akizungumza katika Kipindi cha Tubonge kinachorushwa na Smile FM ya mkoani Manyara leo tarehe 28 Agosti, 2024 ambapo amewaasa wananchi hao ambao watakuwa na sifa za kuandikshwa kujitokeza mara tu zoezi ka uboreshaji wa Daftari utakapoanza mkoani humo.

"Niwaombe wananchi wa mkoani Manyara wenye sifa za kuandikishwa, wale waliohama au wale wanaoboresha taarifa zao kujitokeza mapema na kutokusubiri siku za mwisho ambazo kwa mazoea huwa na watu wengi," amesema Bi.Aswile.
Naye Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Usimamizi wa Uchaguzi, Bi. Saida Hilal amesema kuwa Tume imetoa kipaumbele kwa makundi mbalimbali ya Wazee, wakina mama wenye watoto wachanga wanaonyonyesha (watakaokwenda na watoto wao vituoni), watu wenye ulemavu na wakina mama wajawazito ambao wafikapo katika vituo vya kuandikisha wapiga kura hawatapanga foleni.
Aidha, Bi. Saida ameongeza kwa kusema kuwa Uboreshaji wa safari hii ni tofauti na ule uliopita huku awamu hii kukiwa na mfumo saidizi wa kuboresha taarifa za mpiga kura kwa njia ya mtandao yaani "Online Voter's Registration System" ambao utamsaidia mpiga kura yule anayeboresha taarifa zake kuanza mchakato huo popote pale alipo kwa kutumia simu janja au kiswaswadu.
Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura unatarajiwa kuanza mkoani Manyara tarehe 4 septemba, 2024 hadi tarehe 10 Septemba, 2024 sambamba na mikoa ya Simiyu na Mara.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news