Kamati ya Bunge yatoa maelekezo kwa TAKUKURU na Sekretariati ya Ajira

NA VERONICA MWAFISI

MAKAMU Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria Mhe. Florent Kyombo na Wajumbe wa Kamati hiyo wamezielekeza taasisi za TAKUKURU na Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma kufanya kazi kwa ufanisi ili kujenga imani kwa wananchi juu ya huduma wanazozitoa.
Mhe. Kyombo amesema hayo leo jijini Dodoma wakati wa semina kwa wajumbe wa kamati hiyo iliyotolewa na TAKUKURU kwa kushirikiana na Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma. Semina hiyo ililenga kuwajengea Wajumbe uelewa mpana ili waweze kufanya uamuzi wa masuala mabalimbali kwa maslahi mapana ya nchi. Mhe. Kyombo ameielekeza Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma kutoa elimu kwa wananchi kuhusu namna mchakato wa ajira unavyofanyika ili kuondoa dhana ya wananchi kuwa nafasi za kazi ni kwa ajili ya kundi fulani.
"Wananchi wote wanahaki ya kuomba nafasi ya kulitumikia taifa lao kwa kuomba Ajira Serikalini kupitia Sekretarieti hii, hivyo waelimisheni kuwa mchakato ni wazi kwa yeyote mwenye sifa na akishinda anapata nafasi," alisisitiza Mhe. Kyombo.

Kadhalika Mhe. Kyombo ameipongeza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kwa kuwa na watumishi waadilifu katika utekelezaji wa majukumu yao.
Mhe. Kyombo ametoa wito kwa taasisi hiyo kujikita zaidi katika kuongeza rasilimali fedha na vitendea kazi ili kutoa mchango wenye tija katika kufanya kazi na kufikia lengo la kutoa huduma bora kwa wananchi.

Kwa upande wake, Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deus Sangu ameihakikishia Kamati hiyo kuwa Ofisi ya Rais-UTUMISHI na Utawala Bora kupitia taasisi hizo na taasisi nyingine zilizo chini ya ofisi hiyo zitafanya kazi kwa weledi na ufanisi.
Akitoa neno la shukrani kwa niaba ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, Mjumbe wa Kamati hiyo ambaye ni Mbunge wa Chonga Pemba (ACT), Mhe. Salum Shaafi amezishukuru taasisi hizo kwa kuwapatia mafunzo hayo ambayo yamepanua uelewa wap kuhusu majukumu ya taasisi hizo muhimu kwa taifa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news