LINDI (Agosti 21,2024)-Mahakama ya Wilaya ya Kilwa mkoani Lindi imemtia hatiani aliyekuwa Katibu wa MATANDU AMCOS, Salum Kitengwike katika kesi ya Uhujumu Uchumi Namba 17158/2024.
Salum Kitengwike alikuwa anashtakiwa kwa kosa la kuisababishia hasara mamlaka kinyume na Aya ya 10(1) ya Jedwali la Kwanza pamoja na kifungu cha 57(1) na 60(2) vya Sheria ya Uhujumu Uchumi Sura ya 200 Marejeo ya Mwaka 2002.
Imedaiwa, mshtakiwa kati ya Julai 11,2018 na Julai 14,2018 ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa katika Mkoa wa Lindi, alishindwa kutekeleza majukumu yake kwa usahihi jambo lililopelekea Chama cha Msingi Matandu kupata hasara ya shilingi 13,299,440.
Mshitakiwa kwa uzembe alifanya malipo ya kiasi cha fedha shilingi 13,299,440 kwa mkulima ambaye hakuwasilisha mazao kwenye Chama cha Msingi Matandu.
Wakati wa kusomewa mashtaka upya alisomewa kosa moja kwa mujibu wa makubaliano ambalo ni kosa la kuisababishia hasara mamlaka kinyume na Aya ya 10(1) ya Jedwali la kwanza pamoja na kifungu cha 57(1) na 60(2) vya Sheria ya Uhujumu Uchumi Sura ya 200 Marejeo ya Mwaka 2002.
Mshtakiwa alikiri kosa na kutiwa hatiani kisha kuhukumiwa kifungo jela mwaka mmoja au kulipa faini ya shilingi 100,000 pamoja na kukifidia Chama cha Msingi Matandu hasara ya shilingi 5,000,000 , jumla shilingi 5,100,000.
Mshtakiwa amelipa faini na kufidia Matandu AMCOS ambapo amelipa faini na malipo ya awamu ya kwanza jumla shilingi 2,100,000.
Shilingi 3,000,000 zilizobaki atamalizia kabla ya Desemba 2024 kwa mujibu wa mkataba wa Plea Bargaining.
Aidha,Ofisi ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (TAKUKURU) Mkoa wa Lindi inaendelea na jitihada za kumtafuta mtuhumiwa namba mbili wa tuhuma iliyoanzisha kesi tajwa Bw. Shamte Shabani Mpita.
Mpita akipatikana atafunguliwa shauri la Uhujumu Uchumi kwa Mujibu wa Aya ya 10(1) ya Jedwali la Kwanza pamoja na kifungu cha 57(1) na 60(2) vya Sheria ya Uhujumu Uchumi Sura ya 200 Marejeo ya Mwaka 2002.
Kesi hii imeendeshwa na Wakili wa Serikali, Haruna Ally Mchande wa TAKUKURU Mkoa wa Lindi kwa kushirikiana na Ofisi ya DPO Kilwa.
Tags
Habari
Mahakamani Leo
Matandu AMCOS
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU)
TAKUKURU Tanzania