GEITA-Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi amesema kuwa kazi kubwa anayoifanya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa CCM, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ndiyo namna sahihi ya kumuenzi hayati Dkt. John Joseph Pombe Magufuli.


Vilevile, Balozi Nchimbi alirejea maneno yake hayo wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika katika Uwanja wa Stendi ya Zamani, mjini Chato, akitaja baadhi ya miradi, ikiwemo ujenzi wa Treni ya Kisasa (SGR), Bwawa la Umeme la Mwalimu Nyerere na jinsi ambavyo Serikali inayoongozwa na Rais Samia imeshusha kiasi cha Sh. 123 bilioni kwa ajili ya miradi ya maendeleo katika Wilaya ya Chato.

Balozi Nchimbi amesema kuwa yeye na msafara wa viongozi, wakiwemo Wajumbe wa Kamati Kuu ya CCM aliombatana nao, wamefarijika kufika mahali hapo alipozikwa kiongozi huyo, ikiwa ni mojawapo ya njia ya kumuenzi kwa uongozi wake alioutoa kwa CCM na nchi kwa ujumla.
“Sote ni mashahidi na tunatambua mchango mkubwa wa Hayati Magufuli kwa Chama chetu na nchi yetu. Kazi hiyo kubwa aliyofanya iliashiria uzalendo mkubwa aliokuwa nao. Nitumie nafasi hii kumshukuru sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa CCM, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, hasa kwa kuendeleza miradi yote iliyoachwa na hayati Magufuli, ikiwemo ya Mkoa wa Geita na Chato, kama alivyosema Mbunge,"anasema na kuongeza;
“Kama kuna kitu kizuri katika kumuenzi na kuendeleza kazi kubwa ya Hayati Magufuli ilikuwa ni kuendeleza na kumaliza miradi mbalimbali mikubwa. Hiyo imekuwa ni heshima kubwa kwake Hayati Magufuli, maanza imeendelezwa na kufanyiwa kazi kama ilivyokuwa ndoto zake,” amesema Balozi Nchimbi, wakati wa sala hiyo iliyoendeshwa na Padri Clian Malegeya, kaburini kwa Hayati Magufuli.
Mbali ya kuhani kaburi la Hayati Magufuli, Balozi Nchimbi pamoja na ujumbe wa viongozi wa Chama na Serikali alioambatana nao, na kuwapatia pole familia kwa msiba huo, alipata nafasi ya kumjulia hali Mama yake Hayati Magufuli, Bi. Suzana Musa Magufuli, nyumbani hapo.

Tags
Chama Cha Mapinduzi
Dr Emmanuel John Nchimbi
Dr John Joseph Pombe Magufuli
Dr Samia Suluhu Hassan
Habari