DODOMA-Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amewataka wananchi wa Wilaya ya Bahi na Tanzania kwa ujumla kutambua kazi kubwa inayohitajika ya kutunza vyanzo vya maji ili huduma ya maji safi na salama iweze kuwa endelevu.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akifungua maji mara baada ya kuweka Jiwe la Msingi la Ujenzi wa Mradi wa Maji Ibihwa uliopo Wilaya ya Bahi wakati akiwa ziarani mkoani Dodoma tarehe 19 Agosti 2024.
Makamu wa Rais ametoa wito huo wakati akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Bahi mara baada ya kuweka Jiwe la Msingi Ujenzi wa Mradi wa Maji Ibihwa akiwa ziarani mkoani Dodoma.
Amewahimiza Wakuu wa Mikoa pamoja na Wakuu wa Wilaya kuwaongoza wananchi katika kupanda miti rafiki kwa vyanzo vya maji hususani wakati wa kipindi cha mvua.
Ameitaka Tume ya Umwagiliaji kufanya kazi ya ziada kwa kushirikiana na Wizara ya Mifugo kutengeneza mabwawa ya kuvuna maji katika Mkoa huo kwaajili ya kilimo cha umwagiliaji, mahitaji ya mifugo na binadamu.
Aidha Makamu wa Rais ameiagiza Wizara ya Maji kuhakikisha asilimia 14 za ujenzi wa mradi wa maji Ibihwa zilizobaki zinakamilishwa ifikapo mwisho wa mwezi Septemba 2024.
Pia amesisitiza suala la kufikisha maji ya mradi huo katika maeneo ya Bahi mjini ili kuwasaidia wananchi kuondokana na adha ya maji chumvi wanayopata hivi sasa. Halikadhalika ameagiza kusimamiwa kikamilifu kwa malipo ya mkandarasi wa mradi wa maji Chali – Bahi ili aweze kukamilisha mradi huo.
Makamu wa Rais amesema Mradi wa Maji Ibihwa ni utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi 2020 - 2025, inayolenga kuhakikisha kuwepo kwa usalama wa maji na kuhakikisha huduma ya majisafi na salama inaendelea kuimarishwa na kufikia zaidi ya asilimia 85 ya wakazi wa vijijini na zaidi ya asilimia 95 kwa wakazi wa mijini.
Katika hatua nyingine Makamu wa Rais amekabidhi Ng’ombe (Borani) 20 kwa wafugaji Wilaya ya Bahi zilizotolewa na Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa lengo la kuboresha ufugaji na thamani ya mazao ya mifugo.
Makamu wa Rais ameipongeza Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa mradi huo ambao unatarajia kuongeza kilo za nyama ya ng’ombe kutoka 80-120 wanayopata wafugaji hivi sasa hadi kilo 150 hadi 200 baada mradi.
Makamu wa Rais amewasihi wananchi hususani wafugaji kutambua muhimu kubadili aina ya ufugaji kwa kuanza kufuga kisasa ili kukidhi masoko na viwango vya kitaifa na kimataifa ya mazao ya mifugo yao.
Kwa upande wake Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso amesema Wizara ya Maji itasimamia mradi huo kwa dhamira njema kuhakikisha unakamilika tarehe 30 Septemba 2024.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akinawa mikono kutoka katika maji ya Mradi wa Ibihwa uliopo Wilaya ya Bahi mara baada ya kuweka Jiwe la Msingi la Ujenzi wa mradi huo wakati akiwa ziarani mkoani Dodoma tarehe 19 Agosti 2024.
Ameongeza kwamba kupatikana kwa maji yasiyo na chumvi katika Kijiji cha Ibihwa kumefanya Wizara hiyo kuongeza juhudi za kufikisha maji hayo maeneo mji wa Bahi ambao unakabiliwa na maji ya chumvi.
Mradi wa Maji wa Ibihwa unagharimu shilingi milioni 709 na utatua changamoto ya maji kwa wananchi zaidi ya elfu 11.