Kila Mtanzania ana wajibu wa kushiriki katika zoezi la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura-Waziri Mkuu

KIGOMA-”Zoezi la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura ni muhimu sana katika kuhakikisha nchi yetu inaendelea kuendeshwa kwa misingi ya kidemokrasia;

Kauli hii ilitolewa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa katika hotuba yake ya uzinduzi wa uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura la mkoani Kigoma uliofanyika Julai 20,2024 kwenye uwanja wa Kawawa katika Manispaa ya Kigoma Ujiji.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizindua Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura mkoani Kigoma kwenye uwanja wa Kawawa, Julai 20, 2024. Kushoto ni Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu, Ummy Nderiananga na kulia ni Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji Jacobs Mwambegele. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

Uboreshaji huo utafanyika katika mizunguko 13 na mzunguko wa kwanza unahusisha mikoa mitatu ya Kigoma, Tabora na Katavi kisha Geita na Kagera, ikifuatiwa na Mwanza, Shinyanga na baadae Mara, Simiyu na sehemu ya Mkoa wa Manyara.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo Mheshimiwa Majaliwa alisema kuwa zoezi hilo lina lengo la kuhakikisha wananchi wote wenye sifa wanapata na kutumia haki yao ya kikatiba ya kupiga kura kama ilivyobainishwa kwenye Ibara ya 5 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.

”Vilevile, umuhimu wa zoezi hili unatokana na ukweli kwamba hii ni hatua muhimu ya maandalizi ya kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani utakaofanyika mwaka 2025 hapa nchini. 

"Pia kutokana na uwepo kundi kubwa la wananchi waliopata sifa ya kiumri tangu uchaguzi uliopita, zoezi hili ni muhimu kwa ajili ya kuandikisha wapiga kura wapya”

Akieleza kuhusu umuhimu zoezi hilo Mheshimiwa Majaliwa alisema kuwa,maboresho ya daftari la mpiga kura, mbali ya kuandikisha wapiga kura wapya.

Pia,yanalenga kutoa fursa muhimu kwa wapiga kura ambao kwa sababu moja au nyingine kadi zao za mpiga kura zimepotea au kuharibika au wamehama kutoka eneo moja la uchaguzi kwenda jingine kuboreshewa taarifa zao ili wawe na sifa za kuwawezesha kupiga kura katika uchagu ujao wa Rais, Wabunge na Madiwani.

Aliwataka wote waliohama kutoka kwenye vituo vyao vya kupigia kura nau kupoteza kadi zao kufika kwenye vituo vya kuandikisha wapiga kura ili kuboresha taarifa zao na kupatiwa kadi mpya itakayowawezesha kupiga kura.

Alisisitiza kuwa, kwa mujibu wa takwimu za Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022; inakadiriwa kuwa jumla ya wapiga kura wapya 5,586,433 wataandikishwa wakiwemo waliotimiza umri wa miaka 18 katika kipindi cha kuanzia mwaka 2020.

Ni baada ya uchaguzi mkuu uliopita na ambao watatimiza umri huo ifikapo tarehe ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.

”Kwa mujibu wa taarifa za Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, inakadiriwa kuwa wapiga kura 4,369,531 watboresha taarifa zao.”

"Idadi hii siyo ndogo kwenye zoezi la kupiga kura. Hivyo, nitoe rai kwa kila mpiga kura aliyeandikishwa mwenye uhitaji wa kuboresha taarifa iwe kwa kurekebisha taarifa au kuhama kutoka eneo moja la uchaguzi kwenda lingine asisite kufika katika kituo cha kuandikisha kwani Tume imeshajipanga ili kuhakikisha wananchi wote wanafikiwa."

Mheshimiwa Majaliwa alisema kuwa, ili kufanikisha zoezi hili kila Mtanzania, asasi za kiraia, vyama vya siasa, Jeshi la Magereza na vyuo vya mafunzo, vyombo vya habari, mawakala wa vyama vya siasa na watendaji wa walioteuliwa na tume wanapswa kutimiza wajibu wao ili zoezi hili liweze kufanikiwa.

Wajibu wa kila Mtanzania

Mheshimiwa Majaliwa alisema kuwa, kila Mtanzania ashiriki katika usimamizi wa suala hilo kwani wanaotakiwa kuandikishwa ni raia wa Tanzania tu wenye sifa zilizobainishwa kwa mujibu wa sheria. 

"Wananchi ni watambuzi wa kwanza, niwasihi sana tuwe wazalendo, huu ni wajibu wa raia wa Tanzania kuhakikisha wanaoandikishwa ni Watanzania tu.”

Jeshi la Magereza, vyuo vya mafunzo na Uhamiaji

Hapa Mheshimiwa Waziiri Mkuu anasema kuwa, Uchaguzi wa Serikali za Mitaa pamoja na Uchaguzi Mkuu umeongeza kundi jingine ambalo ni wafungwa wanaotumikia vifungo vya chini ya miezi sita gerezani au kwenye vyuo vya mafunzo na mahabusu hawa wote watapata nafasi ya kupiga kura, hivyo Jeshi la Magereza na upande wa Zanzibar vyuo vya mafunzo wanawajibika kuweka miundombinu wezeshi ili Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi iweze kutekeleza wajibu huo kwa ufanisi.

Aidha, Jeshi la Uhamiaji liwajibike kutoa elimu kwa wananchi kuhusu kuwatambua na kutoa taarifa za uwepo wa mtu au watu ambao siyo raia wa Tanzania, walioandikishwa tayari au wanaopanga kwenda kuandikishwa ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa mapema dhidi yao.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimkabidhi, Josephina Sikabwe kadi ya Mpiga Kura wakati alipozindua Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura mkoani Kigoma kwenye uwnja wa Kawawa, Julai 20, 2024. Kushoto kwake ni Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji, Jacobs Mwambengele. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

Wajibu wa vyama vya Siasa Mheshimiwa Majaliwa anatoa rai kwa viongozi wa vyama vya siasa kuhakikisha mawakala wao wanatoka kwenye mtaa, kijiji na shehia husika ili waweze kutimiza wajibu wao wa kisheria wa kuwatambua watu wenye sifa za kuandikishwa kuwa wapiga kura.

Mawakala wa Vyama vya Siasa

Amesema kuwa kwa upande wa mawakala watakaoteuliwa na vyama vya siasa wanaowajibu wa kutambua watu wenye sifa za kuandikishwa wanaofika kwenye kituo kwa ajili ya kuandikishwa kuwa wapigakura.

Watendaji walioteuliwa na Tume

”Ninawasii sana watendaji walioteuliwa na Tume kuanzia ngazi ya mkoa, jimbo, kata na kituo cha kuandikisha wapiga kura kuwa waadilifu na watangulize uzalendo kwa kutotoa fursa kwa watu ambao hawana sifa za kushiriki katika uboreshaji. 

"Kila mmoja ajitume, afanye kazi kwa weledi na kutumia lugha nzuri wakati kwa wananchi wanaokuja kujiandikisha.”

Taasisi na Asasi za kiraia

Alesema kuwa eneo jingine muhimu ni suala la utoaji wa elimu ya mpiga kura ambapo alizitaka taasisi na asasi zote zilizopewa vibali vya kutoa elimu ya mpiga kura kutekeleza zoezi kwa weledi na wasiingize vitu ambavyo havitakiwi na ambavyo havipo kwenye makubaliano.

”Wakati wa zoezi hili la uboreshaji daftari la mpiga kura , hakikisheni mnatekeleza kazi zenu kwa kuzingatia masharti ya vibali na miongozo iliyotolewa na itakayotolewa na Tume. Ni vema wakati wote ziepuke kufanya masuala ambayo hayamo kwenye miongozo waliyopewa kwa mujibu wa vibali vyao.”

Vyombo vya Habari

Alisema kuwa Vyombo vya habari vinao wajibu wa kutumia kalamu zao, kuwakumbusha wadau wa uboreshaji kutumia taratibu zilizoainishwa kwenye sheria, kanuni na miongozo kutatua au kuwasilisha malalamiko iwapo kutajitokeza changamoto ya aina yoyote wakati wa uendeshaji wa zoezi hili.

“Unapotokea upotoshaji wa aina yoyote, vyombo vya habari viwe vya kwanza kupaza sauti ili kuonesha upotoshwaji huo.”

Kadhalika, Mheshimiwa Majaliwa aliwahakikishia Watanzania kuwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amedhamiria kuhakikisha kuwa Uchaguzi unakuwa wa huru na haki.

Kwa upande wake, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Ummy Nderiandanga amesema kuwa uzinduzi wa uandikishaji na uboreshaji, mchakato huo umeshirikisha wadau mbalimbali wa uchaguzi ikiwa ni utekelezaji wa falsafa ya 4R za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

“Tume imekutana na wadau wa makundi mbalimbali kama vile Vyama vya Siasa, Asasi za Kiraia,Viongozi wa Dini, Makundi Maalum kama vile Vijana, Wanawake na watu wenye Ulemavu.

"Lengo ni kuhakikisha kuwa mchakato huu unakuwa shirikishi kwa watanzania wote bila kujali itikadi za vyama vya siasa au dini.”

Naye, Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Jaji Jacobs Mwambegele alisema kuwa Jumla ya vituo 40,126 vitatumika katika zoezi la uboreshaji wa Daftari ambapo kati ya hivyo, vituo 39,709 vipo Tanzania Bara na vituo 417 vipo Tanzania Zanzibar.

“Idadi hii ya vituo ni ongezeko la vituo 2,312 zaidi ikilinganishwa na vituo 37,814 vilivyotumika kuandikisha Wapiga Kura kwa mwaka 2019/2020."

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news