NA FAUSTINE KAPAMA
Mahakama
KITUO Jumuishi cha Masuala ya Familia Temeke kimepiga hatua kubwa katika kusimamia haki na kutoa huduma bora kwa wananchi tangu kianzishwe mwaka 2021, ikiwemo kusajili na kuamua mashauri ya kifamilia katika ngazi zote za Mahakama na kuhudumia idadi kubwa ya wateja wapatao 526,262.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia Temeke, Mhe. Mwanabaraka Mnyukwa akiwasilisha taarifa ya miaka mitatu ya utendaji kazi wa Kituo hicho kwa Waandishi wa Habari leo tarehe 27 Agosti, 2024.
Akiwasilisha taarifa ya miaka mitatu ya utendaji kazi wa Kituo hicho kwa Waandishi wa Habari leo tarehe 27 Agosti, 2024, Jaji Mfawidhi, Mhe. Mwanabaraka Mnyukwa ameeleza kuwa kumekuwa na mafanikio makubwa yaliyofikiwa tangu kuanzishwa kwake, huku wananchi wakijitokeza kwa wingi kusajili mashauri kila mwaka.
“Mwaka 2021 Kituo kilisajili mashauri 2,383 na kuamua 1,166 na yaliyobaki yalikuwa 1,217. Mwaka 2022 yalisajiliwa mashauri 8,554, yaliyoamuliwa 7,784 na yakabaki 1,987; mwaka 2023 yalifunguliwa mashauri 8,279 na kuamuliwa 8,676, yaliyobaki yalikuwa 1,590. Januari hadi Julai 2024, Kituo kimesajili mashauri 4,993, yaliyoamuliwa ni 4,131 na 2,452 yalibaki,” amesema.
Jaji Mfawidhi amebainisha pia kuwa Kituo Jumuishi Temeke kilipoanzishwa mwaka 2021 hadi 2022 kwa wastani kilikuwa kinapokea wateja 400 hadi 500 kwa siku na idadi hiyo imeongezeka maradufu mwaka 2023 na 2024 ambapo wastani wa wa wateja umepaa na kufikia 800 hadi 1000 kwa siku.
“Tangu kuanzishwa kwa Kituo hadi kufikia tarehe 31 Julai, 2024, kimehudumia wateja wapatao 526,262. Kati ya hao, wanaume wakiwa 228,447, sawa na asilimia 43.4 na wanawake 297,815, sawa na asilimia 56.6 ya wateja wote waliopata huduma kwa kipindi chote,” Mhe. Mwanabaraka amesema katika hafla iliyohudhuriwa pia na Viongozi mbalimbali wa Mahakama.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia Temeke, Mhe. Mwanabaraka Mnyukwa akiwasilisha taarifa ya miaka mitatu ya utendaji kazi wa Kituo hicho kwa Waandishi wa Habari leo tarehe 27 Agosti, 2024. Wengine katika picha ni Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Nkya (kushoto) na Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni, Bi. Mary Shirima.
Viongozi hao ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Gladys Nancy Barthy, Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Nkya, Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni, Bi. Mary Shirima, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu na Katibu wa Msajili Mkuu, Mhe. Jovin Binshanga na wengine.
Amesema kuwa baadhi ya mifumo inayotumika wakati wa usikilizwaji wa mashauri ni Mahakama Mtandao (Virtual Court) ambapo katika kipindi cha mwezi Januari hadi Julai 2024 yamesikilizwa mashauri 370.
Mhe. Mwanabaraka akabainisha kuwa Mahakama Kuu ilisikiliza mashauri jumla ya 124 kutoka katika nchi mbalimbali kama Canada (18), Uingereza (20), Marekani (17), Sweden (7), Denmark (10) na kwingineko mashauri 52.
Kwa upande wa Mahakama ya Wilaya, amebainisha jumla ya mashauri 121 yamesikilizwa kutoka nchi za Canada (21), Uingereza (26), Marekani (31) na kwingineko mashauri 43, huku Mahakama ya Mwanzo ikisikiliza jumla ya mashauri 125 kutoka za Canada (25), Marekani (32), Uingereza (28), China (11) na kwingineko mashauri 29.
“Kwa usikilizwaji wa mashahidi kutoka katika nchi hizi kumeiweza Mahakama kuwapunguzia wananchi gharama za kusafiri na kuwepo mahakamani wakati wa usikilizaji wa mashauri yao pamoja na kuokoa muda ambao wangetumia,” Jaji Mfawidhi amesema.
Hata hivyo, Mhe. Mwanabaraka amebainisha changamoto kadhaa ambazo wamekumbana nazo wakati wa utendaji kazi katika kuhakikisha haki inapatikana kwa wakati katika masuala ya familia, ikiwemo ucheleweshaji wa wananchi kuhamisha mali za marehemu kwenda kwa warithi.
Jaji Mfawidhi amesisitiza kuwa ni wajibu wa msimamizi wa mirathi kugawa mali ya marehemu kwa kuhamisha umiliki wa kila mali, mfano ardhi iwe imepimwa au haijapimwa, hisa, fedha zilizopo katika akaunti za benki, vikundi vya kuweka na kukopa fedha pamoja na magari ili kuweza kugawanywa.
Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania katika Kituo hicho, Mhe. Frank Moshi akitoa utambulisho wa Viongozi mbalimbali waliohudhuria hafla hiyo.
Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania katika Kituo hicho, Mhe. Gladys Nancy Barthy (wa kwanza kulia katika picha ya juu) akiwa na Viongozi mbalimbali wa Mahakama (juu na picha mbili chini) katika hafla hiyo. Picha pia zinaonesha Waandishi wa Habari wakiwa kazini.
“Bado ipo changamoto kubwa ya wateja kutohamisha mali hizo. Katika maadhimisho haya ya miaka mitatu, tumekusudia kukutana na wadau wote wanaohusika na uhamishaji mali za marehemu kwa warithi na kuzungumza nao kuhusu changamoto hii na kutafuta suluhisho la pamoja la kudumu ili mali za marehemu ziende kwa warithi wake kama ilivyokusudiwa,” amesema.
Mhe. Mwanabaraka amebainisha changamoto nyingine ni jamii na wadau kutokuwa na uelewa wa kutosha juu ya masuala ya mirathi na ndoa kwani bado inaamini msimamizi wa mirathi ndiyo mmiliki wa mali za marehemu, hivyo kusababisha mapingamizi hata katika hatua za uteuzi.
Amesisitiza kuwa kazi ya msimamizi wa mirathi ni kukusanya mali na madeni ya marehemu pamoja na kugawa mali hizo kwa warithi wake. Akaeleza kuwa utaratibu wanaotumia katika Kituo ni warithi kupewa fursa ya kujua orodha ya mali ambayo msimamizi wa mirathi ameleta na kuona mgawanyo ili mwenye hoja awasilishe mahakamani kwa mujibu wa Sheria na Taratibu zilizopo.
Changamoto nyingine ni wananchi kutokuwa na uelewa wa kutosha juu ya umuhimu wa uandishi wa wosia kwani kesi nyingi za mirathi zinazofunguliwa kituoni ni zile ambazo marehemu hakuacha wosia na zipo pia baadhi kuna wosia wa jinsi gani mali zake zigawiwe baada ya kufa kwake na kwa watu gani.
“Tumechukua sampuli ya mashauri 118 ambayo yalikuwa na wosia kwa ngazi zote za Mahakama, kati ya hayo, mashauri 95 wosia haukupingwa, hii ni sawa na asilia 80 ya mashauri hayo. Mashauri 23 ambayo ni sawa na asilimia 19 wosia ulipingwa. Miongoni mwa mashauri 23 ambayo wosia ulipingwa ni mawili ambayo ni sawa na asilimia 1.6 na ulibatilishwa…
“Takwimu hizi zinaonesha kuwa uandishi wa wosia unasaidia kuepusha migogoro katika familia mara baada ya mwanafamilia kufariki na hivyo kuongeza kasi ya haki mirathi na kuweka udugu na upendo kwa wadaawa,” Jaji Mfawidhi amesema.
Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia Temeke kinajumuisha Mahakama nne, ikiwemo Mahakama Kuu iliyoanzishwa kupitia Tangazo la Serikali Na. 640/2021, Mahakama ya Wilaya iliyoanzishwa kwa Tangazo la Serikali Na. 641/2021 na Mahakama ya Mwanzo iliyoanzishwa kwa Tangazo la Serikali Na. 639/2021.
Matangazo haya yote yalitolewa tarehe 27 Agosti, 2021. Aidha, Kupitia Tangazo la Serikali Na. 794 la 2023 imelifanyia marekebisho Tangazo la Serikali Na.640/2021 na kuwepo kwa usimamizi wa masuala ya madai katika Mahakama ya Mtoto ya Dar es Salaam chini ya Masijala ya Temeke.