Kuweni na matumizi bora ya fedha kuepuka mikopo isiyo rasmi-Dkt.Mussa

NA RAMADHAN KISSIMBA
WF Morogoro

KATIBU Tawala wa Mkoa wa Morogoro, Dkt. Mussa Ally Mussa, amewataka wajasiriamali wa mkoa huo kuwa na matumizi bora ya fedha wanazozipata katika shughuli zao mbalimbali za uzalishaji mali ili kuepukana na mikopo isiyo rasmi (mikopo umiza).
Afisa Usimamizi wa Fedha kutoka Wizara ya Fedha, Bw. Stanley Kibakaya akiwaelekeza wafanyabiashara wa Soko la Chifu Kingalu lililopo Mkopo Morogoro, jinsi ya kupakua filamu maalumu ya kutoa elimu ya fedha.(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Wizara ya Fedha, Morogoro).

Dkt. Mussa alisema hayo wakati wa kikao na timu ya kutoa elimu ya fedha kwa Umma kutoka Wizara ya Fedha ambayo ipo Mkoani Morogoro kutoa elimu hiyo kwa makundi mbalimbali ya wananchi katika halmashauri saba (7) za mkoani wa Morogoro.

‘’Shida moja niliyoigundua kwa wananchi wetu wa Morogoro wanaweza wakapewa mkopo, na pengine hawana haja ya kupewa mkopo kutokana na kipato chao, lakini kipato chenyewe kinatumika vibaya na kikitumika vibaya inawasababishia kuwa na mikopo isiyotarajiwa hasa ile ya kinyonyaji’,’ alisema Dkt. Mussa.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro, Dkt. Mussa Ally Mussa, akiongea na timu ya program ya kutoa elimu ya fedha kwa Umma (haipo pichani) katika kikao kilichofanyika ofisini kwake mkoani Morogoro.

Dkt. Mussa aliwataka waratibu wa program ya elimu hiyo pamoja na yale waliyokusudia kuwaelimisha wananchi kuhusu program ya utoaji elimu ya masuala ya fedha, wakumbuke pia kuwaelimisha kuhusu matumizi ya rasilimali walizonazo ambazo zitawasaidia kuboresha maisha yao kupitia shughuli mbalimbali za kiuchumi na hatimaye kuwaepusha na mikopo ya kinyonyaji.
Mwenyekiti wa Wafanyabiashara wa Soko la Chifu Kingalu la Mkoani Morogoro, Bw. Khalid Mkunyegele, akizungumza na wafanyabiasha wa soko hilo (hawapo pichani) kabla ya kumkaribisha mratibu wa program ya kutoa elimu katika ukumbi wa mikutano wa soko hilo.

Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro kupitia kikao hicho aliwaasa wananchi wa Halmashauri zitakazotembelewa na timu kuhakikisha hawakosi fursa hiyo ya kupata elimu ya masuala ya usimamizi wa fedha binasfi, uwekaji wa akiba, mikopo na mengineyo ambayo itawasaidia katika maisha ya baadaye.
Afisa Usimamizi wa Fedha kutoka Wizara ya Fedha, Bw. Stanley Kibakaya, akizungumza na wafanyabiashara wa soko la Chifu Kingalu – Mkoani Morogoro (hawapo pichani) kuhusu umuhimu wa kuweka akiba na matumizi bora ya fedha zinazotokana na biashara zao.

Awali akizungumza kwenye kikao hicho, Afisa Usimamizi wa Fedha kutoka Wizara ya Fedha Bw. Stanley Kibakaya, alisema kuwa lengo la Wizara kutoa elimu hiyo ni kujaribu kuwahiza wananchi wa Mkoa wa Morogoro na Tanzania kwa ujumla kuhakikisha pesa wanayoipata kutokana na uzalishaji mbalimbali wanaoufanya wanaiwekeza kwa ajili ya matumizi ya baadae.

Aidha, Bw. Kibakaya aliongeza kuwa program ya elimu ya fedha italenga pia watoa huduma ya fedha kwa kuwahimiza kutoa huduma hizo kwa kufuata sheria na miongozo iliyotolewa na Benki Kuu ya Tanzania na Taasisi ambazo hazijajirasimisha kufanya hivyo ili wapatiwe leseni itakayowawezesha kufanya shughuli za utoaji wa huduma ndogo za fedha kwa kuzingatia sheria.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro, Dkt. Mussa Ally Mussa (Katikati) akiwa katika picha ya pamoja na timu ya watalaamu wa program ya kutoa elimu ya fedha kutoka Wizara ya Fedha na wadau wa sekta ya fedha nchini mara baada ya kikao na Katibu Tawala kilichofanyika mkoani Morogoro.

Programu ya kutoa elimu ya Fedha kwa umma Mkoani Morogoro itafanyika katika Halmashauri ya Morogoro Mjini, Morogoro vijijini, Kilosa, Mvomero, Ifakara, Mlimba na Gairo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news