DODOMA-Msajili wa Hazina,Nehemiah Mchechu amesema, lengo kuu la maboresho yanayoendelea ndani ya taasisi na mashirika ya umma nchini ni kuzifikisha taasisi hizo kwenye Soko la Hisa.
Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu (katikati) akiwa na Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF, Bw. Abdul -Razaq Badru (kulia) na Mkurugenzi Mkuu wa WCF, Dkt. John Mduma baada ya kuingia ubia wa kumiliki Kiwanda cha Chai cha Mponde.
Ameyasema hayo baada ya Ofisi ya Msajili wa Hazina (TR) kwa kushirikiana na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), pamoja na Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) kuingia ubia wa kumiliki Kiwanda cha Chai cha Mponde kwa ajili ya kuongeza tija katika uzalishaji.
Vile vile,wadau mbalimbali wametakiwa kuchangamkia fursa ya uwekezaji katika zao la chai.
Katika ubia huo Ofisi ya Msajili wa Hazina kwa niaba Serikali inamiliki hisa ya asilimia 16, huku PSSSF na WCF wanamiliki asilimia 42 kila mmoja jambo ambalo litaongeza kasi ya utendaji katika ushindani wa soko na kufanya Taifa kupata gawio kama ilivyo kwa taasisi nyingine.
Akizungumza jijini Dodoma Agosti 9, 2024 katika hafla ya utiaji saini makubaliano ya kumiliki kiwanda hicho iliyofanyika katika Ofisi ya PSSSF, Msajili wa Hazina,Bw. Nehemia Mchechu, amesema kuwa uwekezaji huo unakwenda kuongezeka thamani ya kiwanda na kufikia shilingi bilioni 4.8.
"Serikali inatarajia kuongeza uwekezaji wake katika Kiwanda cha Chai cha Mponde kufikia shilingi bilioni 4.8 kutoka bilioni 2.5 za sasa, lengo ni kuimarisha soko la zao la chai na uchumi wa wakulima na wakazi wa Wilaya za Lushoto na Korogwe."
Msajili wa Hazina,Nehemiah Mchechu akizungumza katika hafla hiyo iliyofanyika Agosti 9,2024 jijini Dodoma.
Kuhusu maboresho, Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu amesema kuwa,"Kwanza ni kuhakikisha hizi reforms tunazosimamia zinakwenda haraka na pale ambapo reforms imefanikiwa, then kuipeleka taasisi husika kwenye Soko la Hisa.
"Unapopeleka kwenye Soko la Hisa tunategemea wawekezaji wadogo wadogo, lakini pia wawekezaji wakubwa na ndiyo focus yetu tunapokwenda."
Mchechu ameongeza kuwa, walikuwa na mkupuo wa taasisi nyingi ambazo nyingine zilienda sekta binafsi na nyingine Soko la Hisa
kwa kipindi fulani.
"Lakini,labda kwa kusimamiwa au kuongozwa na World Bank na mashirika makubwa ya kifedha, tukasema hapana kwa sasa hivi Mheshimiwa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan yeye mwenyewe kwa maono yake amesema anataka haya yafanyike.
"Kwa hiyo, ninafikiri tutakuwa na makampuni ya kutosha yanaoingia kwenye Stock Markets, tunachotarajia ni sisi katika zile reforms tulizozianza mwaka jana na mwaka huu wa fedha tuutumie kuangalia vizuri na ku-analyisis tuangalie ni taasisi zipi ambazo zimeanza ku-transforms."
Amesema, wanaweza kuwa na taasisi chache au nyingi katika mwaka ujao wa fedha au mwishoni mwa mwaka huu katika kuyaendea malengo hayo.
Wakati huo huo, Mchechu amesema Kiwanda cha Chai Mponde kinakwenda kufufua uchumi kwa wakazi wa Korogwe mkoani Tanga na wakulima wa zao la chai watapata fursa ya kupata soko la uhakika ili kuuza mazao yao.
Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu (katikati) akiwa na Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF, Bw. Abdul -Razaq Badru (kulia) na Mkurugenzi Mkuu wa WCF, Dkt. John Mduma wakisaini makubaliano ya kuingia ubia wa kumiliki Kiwanda cha Chai cha Mponde.
Amesema kupitia uwekezaji huo, Serikali inakwenda kunufaika na ulipaji wa kodi, huku akisisitiza umuhimu wa menejimenti kuongeza ufanisi katika utendaji ili waweze kuleta gawio kama ilivyo kwa taasisi nyingine nchini.
Vile vile, Mchechu amewashukuru PSSSF, WCF kwa kukubali wito wa kwenda kufanya uwekezaji katika sekta ya kilimo cha chai.
"Ukiangalia tuna ardhi nzuri ambayo tunaweza kufanya uwekezaji kwenye maeneo mbalimbali nchini.PSSSF na WCF wanapoonekana katika uwekezaji sekta ya kilimo itawavutia wadau wengine na kufanya vizuri sekta hii, kwani kwa muda mrefu wakulima walishindwa kulima zao la chai kutokana na kukosa soko la uhakika.”
Tags
Habari
Kiwanda cha Chai Mponde
Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF)
Ofisi ya Msajili wa Hazina
PSSSF Tanzania