DAR-Shirika la Reli Tanzania (TRC) limeomba radhi kwa abiria waliosafiri kutoka Dodoma saa 2.15 usiku kuelekea Dar es Salaam Agosti 1, 2024 kwa treni ya mwendo kasi kuchelewa kuwasili kutokana na hitilafu ya kiufundi iliyotokea eneo la Mtaa wa Mshikamano Kata ya Kihonda mkoani Morogoro.
Taarifa iliyotolewa na Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano wa TRC, Jamila Mbarouk tarehe 2 Agosti 2024 imeeleza kuwa, hitilafu za kiufundi zilitokea majira ya saa 4.33 usiku na kushughulikiwa kwa muda wa takribani saa moja na kusababisha treni hiyo ya abiria kutoka Dodoma kuchelewa kuwasili Dar es Salaam kwa wakati uliopangwa.
Aidha,TRC imetoa taarifa kuwa treni ya abiria iliyobeba viongozi na wananchi wengine waliotoka Dodoma saa 1 usiku baada ya kushiriki sherehe za uzinduzi wa SGR iliwasili Dar es Salaam kwa muda uliopangwa bila hitilafu yeyote.
Halikadhalika TRC imeeleza kuwa inazingatia usalama wa abiria kabla na wakati wa safari ili kuepusha madhara kwa watumiaji wa huduma za usafiri wa reli na linaomba radhi kwa usumbufu uliojitokeza.
Tags
Kurasa za Magazeti
Kurasa za Mbele na Nyuma za Magazeti
Magazeti
Magazeti ya Leo
Magazetini
Magazetini leo
Yaliyojiri Magazetini Leo