Mahakama ya Tanzania yarekodi mafanikio ya namna yake

NA FAUSTINE KAPAMA
Mahakama Morogoro

MABORESHO yaliyofanywa na yanayoendelea kufanyika mahakamani hayatafikiwa na taasisi yoyote ndani ya Serikali au nchi jirani kwa muda wa miaka 20 ijayo.
Jaji wa Mahakama Kuu na Mkuu wa Kitengo cha Maboresho cha Mahakama ya Tanzania, Mhe. Dkt. Angelo Rumisha akisisitiza jambo alipokuwa anaongea na Waandishi wa Habari mkoani Morogoro kuhusu hali ya utekelezaji wa mikakati na miradi ya maboresho katika utoaji huduma ndani ya Mahakama ya Tanzania.

Hayo yamebainishwa na Jaji wa Mahakama Kuu na Mkuu wa Kitengo cha Maboresho cha Mahakama ya Tanzania, Mhe. Dkt. Angelo Rumisha alipokuwa anaongea na Waandishi wa Habari mkoani hapa kuhusu hali ya utekelezaji wa mikakati na miradi ya maboresho katika utoaji huduma ndani ya Mahakama ya Tanzania.

“Tunayofanya sisi hatutalinganishwa na mtu yoyote, hakuna atakayetufikia kwa miaka 20 ijayo, iwe ndani ya Serikali au majirani zetu,” Mhe. Dkt. Rumisha amesema kwenye mkutano huo uliofanyika leo tarehe 30 Agosti, 2024 katika Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Morogoro.

Amesema kuwa hakuna mbadala, zaidi ya kuboresha huduma kwa sababu ni haki ya wananchi kupata na kujua haki zao, hivyo ni muhimu kwa Taasisi na wadau wengine kuboresha huduma zao ili waende sambamba na kile kinachofanyika mahakamani.
Mkuu wa Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano cha Mahakama ya Tanzania, Ndugu Gerald Chami akitambulisha Viongozi mbalimbali wa Mahakama waliohudhuria mkutano huo.

Mhe. Dkt. Rumisha alitoa mfano eneo moja la mlundikano wa mashauri kati ya maboresho mengi ambayo Mahakama ya Tanzania imepiga hatua kubwa katika kuharakisha utoaji wa haki kwa wananchi.

Alieleza kuwa kwa sasa mlundikano wa mashauri kwa Mahakama nchi nzima ni asilimia tatu ya mashauri yote, huku akibainisha kuwa hakuna mlundikano katika ngazi ya Mahakama za Mwanzo.

“Kwenye asilimia 70 ya mashauri yote yanayosikilizwa mahakamani, hakuna kesi ambayo imezidi miezi sita tangu kufunguliwa. Kwa hiyo, mlundikano ni asilimia sifuri. Ebu muulize jirani yetu yoyote kuhusu mlundikano au taja nchi yoyote ujue ni asilimia ngapi,” amesema.

Mhe. Dkt. Rumisha aliwaeleza Waandishi wa Habari kuwa mwezi wa pili mwaka 2024, kuna majirani walimuuliza Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma miujiza gani ambayo Mahakama ya Tanzania imefanya kufikia mafanikio hayo, ikiwemo kumaliza mlundikano wa mashauri mahakamani.
Amebainisha kuwa, majirani hao waliomba mtumishi anayeshughulikia masuala ya maboresho kwenda kuwasaidia ambapo Jaji Mkuu alimtuma yeye kama Mkuu wa Kitengo cha Maboresho na kuzungumza nao na walikuwa hawaelewi miujiza iliyofanyika.

“Kwetu shauri linakuwa la mlundikano likizidi miezi sita tangu kufunguliwa, wenyewe ni miaka miwili Mahakama ya Mwanzo na kwao asilimia 47 zimezidi miaka miwili katika Mahakama za Mwanzo. Huwezi kujua kimo changu mpaka ujue kina cha shimo niliposimama,” amesema.

Jaji Rumisha aliwaomba Waandishi wa Habari kuangalia viwango vya uondoshaji na umalizaji wa mashauri ambazo ndiyo viashiria vya utendaji kazi wa Mahakama na kulinganisha kile Mahakama ya Tanzania inachokifanya na nchi nyingine, kwani ukweli lazima usemwe.

Akizungumzia maendeleo ya miundombinu ya majengo, Mhe. Dkt. Rumisha ameeleza kuwa kwa sasa kuna Mahakama za Mwanzo na Mahakama za Wilaya 60 ambazo zinaendelea kujengwa na zinatarajiwa kukamilika ifikapo Februari, 2025.

Alieleza pia kuwa kuna Vituo Jumuishi vya Utoaji Haki vipya tisa vinajengwa katika Mikoa ya Katavi, Songwe, Njombe, Songea, Lindi, Geita, Simiyu, Singida na Visiwani Pemba, kwani kukamilika kwake kutafanya huduma ya Mahakama Kuu kupatikana nchini kwa asilimia 100.

Kuhusu mifumo mbalimbali inayorahisisha huduma za kimahakama, Mhe. Dkt. Rumisha amebainisha kuwa kwa sasa Mahakama ya Tanzania ina mifumo 16, ikiwemo ule unaochapisha maamuzi katika mtandao (TanzLii) ambao umerahisisha upatikanaji wa nakala za hukumu na ufanyaji wa tafiti kufanyika kwa urahisi, hivyo kuchangia utoaji wa haki kwa wakati.

“Tunakitu kinaitwa Situation Room ambayo inaonesha kila kitu kinachofanyika mahakamani kwa wakati huo kwa nchi nzima. Mfumo huu unapatikana nchi mbili tu Duniani, Tanzania na Kazakhstan,” amesema.
Sehemu ya Waandishi wa Habari wakimsikiliza Jaji wa Mahakama Kuu na Mkuu wa Kitengo cha Maboresho cha Mahakama ya Tanzania, Mhe. Dkt. Angelo Rumisha na kuchukua matukio mbalimbali kwenye mkutano huo.

Amefafanua pia kuwa licha ya kuwasaidia Viongozi wa Mahakama kujua kinachofanyika katika kila Mahakama nchini kwa wakati husika, mfumo huo pia unasaidia kuzalisha data zinawezesha kufanya maamuzi ndani ya Mahakama, ikiwemo upangaji wa watendaji.

Mhe. Rumisha ameeleza kuwa Mahakama ya Tanzania imeondoa kabisa malalamiko ya wananchi ya kupata hukumu kwa lugha ya Kiswahili kutoka katika lugha ya Kiingereza kwa uanzisha mfumo wa unukuzi na tafsiri ambao pia unaowasaidia Majaji na Mahakimu kuendesha mashauri bila kuandika kwa mkono.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news