Makamu wa Rais aiagiza Wizara ya Fedha kutoa kipaumbele cha fedha ujenzi VETA Mpwapwa

DODOMA-Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango ameiagiza Wizara ya Fedha kutoa kipaumbele katika mradi wa Ujenzi wa Chuo cha Veta Wilaya ya Mpwapwa ili wananchi wa wilaya hiyo na maeneo jirani kunufaika na mafunzo ya ufundi na ujuzi.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akisikiliza maelezo kutoka kwa Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda wakati alipotembelea mradi wa ujenzi wa Chuo cha Veta Mpwapwa kinachojengwa eneo la Kibakwe akiwa ziarani mkoani Dodoma tarehe 20 Agosti 2024.

Makamu wa Rais ametoa maagizo hayo mara baada ya kutembelea mradi wa Ujenzi wa Chuo cha Veta Mpwapwa unaojengwa katika Jimbo la Kibakwe akiwa ziarani mkoani Dodoma.

Amesema vyuo hivyo vya ufundi ni fursa kwa vijana katika kupata mafunzo ya kiujuzi na hivyo kuweza kujiajiri. Mradi huo unagharimu shilingi bilioni 1.68.

Awali akizungumza na wananchi wa Kibakwe Makamu wa Rais amekemea uharibifu uliofanywa katika msitu wa mlima wotta uliopo Wilaya ya Mpwapwa.

Amemuagiza Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) kwa kushirikiana na Waziri wa Maliasili na Utalii pamoja na Waziri wa Ardhi kutembelea eneo hilo na kuhakikisha wanaweka utaratibu wa kudhibiti uharibifu unaoendelea.
Pia Makamu wa Rais ameiagiza Wizara ya Ujenzi kupitia Wakala ya Barabara nchini (TANROAD) kuharakisha mchakato majadiliano na mapitio ya hatua za mwisho za manunuzi ili kumpata mkandarasi wa barabara kiwango cha lami Mpwapwa - Kibakwe (Km 46.5) pamoja na kukamilisha usanifu wa barabara ya Kibakwe – Chipogolo (Km 84) ili ziweze kujengwa na kuowaondolea changamoto ya miundombinu wananchi wa Wilaya ya Mpwapwa.

Amewataka pia kusimimia kikamilifu utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa barabara kiwango cha lami kilometa 32 ya Kongwa – Mpwawa ili iweze kukamilika kwa wakati.

Mapema akizungumza na wananchi wa kata ya Rudi akiwa katika ziara hiyo Wilaya ya Mpwapwa, Makamu wa Rais ameiagiza Wizara ya Maji kupeleka gari la kuchimba visima katika kata hiyo kabla ya tarehe 15 Septemba ili kuchimba visima katika vijiji viinavyokosa maji katika kata hiyo.
Aidha, Makamu wa Rais amewahimiza wananchi wa kata ya Rudi kuweka mkazo katika kuhakikisha watoto wanapata elimu ikiwemo kufuatilia elimu hiyo wanayoipata. Amesema ili Taifa liweze kupata maendeleo ya haraka linahitaji jamii iliyopata elimu katika nyanja mbalimbali.

Amewasisitiza wazazi na walezi katika kata hiyo kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa kuweka mpango bora wa wanafunzi kupata chakula wakiwa shuleni hali itakayosaidia watoto hao kupata elimu kwa utulivu.

Akiwa katika ziara Wilaya ya Mpwapwa, Makamu wa Rais amewasisitiza wananchi kutambua umuhimu wa kushiriki katika uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika mwezi Novemba hiyo ikienda sambamba na kujiandikisha katika daftari la kupiga kura.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akisikiliza maelezo kutoka kwa Msimamizi wa Ujenzi QS Sadick Sibora kuhusu maendeleo ya ujenzi wa mradi wa Chuo cha Veta Mpwapwa kinachojengwa eneo la Kibakwe wakati alipotembelea mradi huo akiwa ziarani mkoani Dodoma tarehe 20 Agosti 2024.

Aidha amewasihi kushiriki katika siasa kwa ustaarabu bila vurugu na kutunza amani iliyopo kwa manufaa ya vizazi vya sasa na baadaye.

Makamu wa Rais anaendelea na ziara ya kikazi ya siku nne mkoani Dodoma ambapo anakagua miradi mbalimbali ya maendeleo, kuzindua miradi iliyokamilika pamoja na kusikiliza kero za wananchi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news