Makamu wa Rais aridhishwa na utendaji wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji,asema yajayo ni mema zaidi

DODOMA-Makamu wa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt.Philip Mpango amesema uwekezaji unaofanywa na Serikali katika Sekta ya Umwagiliaji unaenda kuandika historia ya kumaliza tatizo la njaa nchini na kulijengea Taifa heshima kupitia uwepo wa chakula cha kutosha.
Amesema, anaridhishwa na kazi kubwa inayofanywa na Tume ya Taifa ya Umwagiliaji chini ya Wizara ya Kilimo, hivyo wananchi wawe tayari kuipokea miradi hiyo mikubwa sekta ya umwagiliaji itakayomaliza tatizo la uhaba wa chakula na kuimarisha kilimo cha uhakika nchini.

Dkt. Mpango amesema hayo leo katika ziara yake mkoani Dodoma wakati wa uwekaji wa jiwe la Msingi katika ujenzi wa Shamba la Pamoja la Dkt. Samia Suluhu Hassan (Dkt.Samia Suluhu Hassan Block Farm) ambao unaotekelezwa na Tume ya Taifa ya Umwagiliaji ukiwa na thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 21.7

“Hapa Dodoma kuna salamu ya Mkuliachi ambayo ni salamu na inamaanisha njaa, niwahakikishie kuwa hiyo salamu inaenda kuisha kupitia uwekezaji unafanywa na serikali,katika miradi hii mikubwa ya umwagiliaji inaenda kuandika historia ya kumaliza tatizo la njaa nchini na kulijengea Taifa heshima ya uwepo wa chakula cha kutosha.

“Niwashukuru wananchi wa maeneo ya mradi kwa kuridhia kutoa ardhi yao na kazi kubwa inayofanywa na Tume chini ya Wizara ya kilimo katika kufanikisha miradi hii,”amesema.

Aidha, Dkt. Mpango amesisitiza kuwa, Tume ya Taifa ya Umwagiliaji.inafanya kazi kubwa na hatua hiyo ndio maana ya kubadili mifumo sekta ya kilimo na kuwa na kilimo chenye tija na cha uhakika.

“Nawapongeza sana,hili litakuwa ni eneo la mfano na mashamba haya yawe mashamba darasa,elimu ya kilimo itolewe hadi kwa vijana hususani vitendo siyo maneno.”

Alitumia fursa hiyo kusifu hatua ya mradi huo kuhusisha ujenzi wa kituo cha afya na barabara yenye urefu wa zaidi ya kilomita 18.8 umbapo ujenzi huo unatekelezwa na Tume ya Taifa ya Umwagiliaji.

Aidha,Dkt.Mpango ameagiza eneo la barabara lililobaki ambalo lipo chini ya Wakala wa Barabara Vijijini (TARURA) litekelezwe na Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) na kuwapo na miundo mbinu ya uhakika ya mawasiliano katika vijiji hivyo vya mradi.

Dkt. Mpango alihitaji kufahamu mazao yaliyopangwa kulimwa katika eneo la mradi ambapo Mtaalamu wa Kilimo kutoka wizara ya Kilimo alibainisha kuwa mazao yatakayo limwa katika eneo la mradi ni pamoja na Soya,Mtama,Alizeti pamoja na Mahindi.
Mapema akimkaribisha na kutoa ufafanuzi juu ya Mradi huo, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, Raymond Mndolwa amesema, nradi una ukubwa wa julma ya hekari 11,000 na umekusudiwa kuleta manufaa ya moja kwa moja kwa Halmashauri ya Chamwino na vijiji vyake.

Ni kupitia ujenzi wa nyumba za vijana, uwekaji wa miundombinu katika eneo la hekari 1000 za jijiji pamoja na uandaaji wa zaidi ya hekari 400 katika eneo la mradi wa umwagiliaji wa vijana, ambapo eneo lote linawekewa miundombinu ya umwagiliaji.

Kwa mujibu wa Mndolwa, kila kijana mnufaika wa mradi atapewa hekari 10 na kwamba mpaka sasa nyumba 60 za makazi ya vijana zimeshakamilika kwa asilimia 50.

Mndolwa pia ameongeza kuwa, tume imepewa jukumu la kuandaa maeneo ya michezo, maghala na huduma nyingine za jamii na Kila kijana atapewa hekari kumi na kwamba kuna uchimbaji wa visima 11 ambapo visima 7 vimesha chimbwa na kwamba kutakuwepo pia na ujenzi wa jengo la utoaji huduma za kilimo (Farm House) katika eneo la mradi.

Amebainisha kuwa eneo la mradi lina maji mengi ya mvua lakini Tume imejipanga kutumia vyanzo vingine vya maji kupitia uchimbaji wa visima Pamoja na ujenzi wa bara bara zitakazo weza kupitika kipindi chote cha mwaka.

Naye Naibu Waziri wa Kilimo,David Silinde, amasema wizara imeelekeza halmashauri zote nchini kutenga maeneo yatakayo tumika kwa ajili ya ujenzi wa miradi ya vijana na Wizara itafanya kazi ya ujenzi wa miundombinu ya Umwagiliaji na kwamba katika eneo la Mradi wa Shamba La Pamoja la Mama Samia, serikali imetenga hekari 1000 kwa ajili ya Mradi wa Umwagiliaji wa Kijiji na kwamba Halmashauri ya Chamwino pia imetengewa eneo la umwagiliaji

Aidha, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Rosemary Senyamule, aliishukuru serikali kwa uwekezaji Mkubwa unaofanywa na serikali ndani ya Mkoa wa Dodoma, ambapo asilimia 72 ya wakazi wake wanategemea kilimo.

”Tumewekewa miundo mbinu ya umwagiliaji na sasa tunauhakika wa kupata Lishe bora,ajira zitaongezeka na uchumi wa mkoa utakuwa.”

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Chamwino, David Lusinde amesema kwa sasa wananchi wa Chamwino wametoka katika kuzungumzia ukame na sasa wanazungumzia habari za maendeleo ya kilimo kupitia umwagiliaji na anaamini kuwa ukame ulikuwa katika fikra za watu.

Lusinde pia amesema Ndogowe na Mlazo watakuwa washiriki na siyo watazamaji, na kwamba Wafugaji wa Chamwino pia wapo na wanatambulika katika eneo hilo la mradi

Mradi wa Shamba la Pamoja la Mama Samia unajengwa katika kata ya Mlazo Halmashauri ya Chamwino mkoani Dodoma ambapo upo kilomita 100 kutoka barabara kuu ya Dodoma Iringa.

Mradi huu ni sehemu ya Mpango wa Serikali ya Awamu ya Sita kuwainua vijana kiuchumi kwa kuwawezesha vijana kujiajiri kupitia kilimo cha umwagiliaji.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news